Udhaifu Wa Imani… Alama Zake, Sababu Na Matibabu Yake

Utangulizi:

Udhaifu wa Imani ni ugonjwa ulioenea sana miongoni mwa Waislamu, na ni ugonjwa wa hatari kuliko magonjwa yote ambayo anaweza kuyapata Muislamu, kwa sababu ni ugonjwa unaoshambulia ‘Aqiydah yake, unaoharibu uhusiano baina yake na Muumba wake.

Ugonjwa huu ni hatari kwani humshambulia mtu pasi na yeye kujua wakati mwingine, bali huhisi tu athari zake za kuwa na moyo uliosusuwaa (mgumu), kutohisi ladha ya ibada zake, kutoathirika na Qur-aan na mawaidha, kuteleza kwenye maasi kwa wepesi, kutowapenda watu wa kheri na wanaoamrisha mema na kukataza maovu, na athari nyingine nyingi.

Ugonjwa huu huingia katika moyo wa Muislamu, kwani ndio kiungo muhimu lakini dhaifu, kiungo ambacho kina sifa ya kugeuka geuka na kubadilika kutoka hali kwenda hali nyingine kwa wepesi mkubwa, kama kilivyosifiwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

“Hakika Moyo umeitwa moyo kwa kugeuka kwake, kwani mfano wa moyo ni mfano wa unyoya ulionin’ginia katika tawi la mti unapeperushwa na upepo huku na kule” Imam Ahmad katika As-Swahiyh Al Jaami’i.

Na katika mafundisho mengine ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameusifia moyo kuwa ni wenye kugeuka kwa haraka sana kushinda hata maji yanayotokota pale aliposema:

“Moyo wa Mwanaadamu unageuka haraka kuliko hata chungu kinapotokota)” Imaam Ahmad.

Na ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa katika du’aa zake alizokuwa anapenda kuziomba kama tunavyosimuliwa na ‘Abdullaah bin ‘Amru bin Al-‘Aasw kuwa alimsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

“Hakika nyoyo za wanaadamu zote zipo katika vidole viwili miongoni mwa vidole vya Ar-Rahman kama moyo mmoja, Anazigeuza Atakavyo) kisha Mtume akaomba du’a kwa kusema:

“Ewe Mwenye kuzigeuza nyoyo, zigeuze nyoyo zetu zielekee kwenye kukutii” Muslim

 

Baada ya utangulizi huo, hebu sasa tuangalie alama za udhaifu wa imani, sababu zake na jinsi ya kutibu ugonjwa huu.

1.     Kutenda Ma’aswiy: Ma’aswiy ni moja ya alama kubwa za udhaifu wa imani ya mja, na kila mtu anvyozidi kufanya ma’aswiy ndio imani yake inavyozidi kudhoofika na ndiyo anavyozidi kuzama ndani ya vilivyo haramishwa na kutoona aibu kujifakharisha na matendo hayo. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametoa makaripio makali sana pale aliposema: “Umma wangu wote watapata msamaha isipokuwa wale wanadhihirisha, na hakika miongoni mwa kudhihirisha ni mtu kufanya tendo usiku, kisha anaamka asubuhi hali ya kuwa Allaah Amemsitiri na akasema: Ewe Fulani, jana nilifanya kadhaa wa kadhaa. Alilala hali ya kuwa Allaah amemsitiri, lakini alipoamka akanza kutoa siri Alizositiriwa na Allaah.” Al-Bukhaariy.

 

2.     Kususuwaa kwa Moyo: moyo unapokuwa mgumu mpaka unakuwa kama jiwe, mja hujikuta haathiriki na chochote katika nafsi yake. Mwenye moyo mgumu haathriki hata na mauti ambayo ni mawaidha tosha, bali unaweza kumkuta makaburini akimzika ndugu yake na wakati huo huo akipanga mambo ya kumuasi Allaah. Wengine utawakuta wakitoa vichekesho na mizaha, watu wa aina hii wanakuwa ni mfano wa jiwe lisioathirika, Allaah Anasema: “Kisha nyoyo zenu zikawa ngumu baada ya hayo (yote), zikawa kama mawe au ngumu zaidi (ya mawe)” 2: 74.

 

3.     Kutofanya Ibada kwa ufanisi: Mwenye imani dhaifu hufanya ibada zake kwa kuripua, hajali kabisa ufanisi na nidhamu katika ibada. Utaona anaswali bila utulivu, anatembeza macho huku na kule, anakwenda miayo hovyo, anaswali kwa uvivu kama vile kalazimishwa, na sifa hii inafanana na sifa za wanafiki katika kufanya ibada zao, kwani wao hawajali ile roho na undani wa ibada bali hujali zaidi kuonekana. Allaah Anasema: “…Na wanaposimama kuswali, husimama kwa uvivu…” 4: 142. Na daima utamkuta anachelewa Swalah za Jama’ah na kupuuzia mambo ya Sunnah kwa kuyaona madogo hayana umuhimu wowote, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: “Hawatoacha watu kuchelewa Swaffu ya mwanzo (katika Swalah) mpaka Allaah Awatie motoni.” Abu Daawuud.

 

4.     Kutoathirika na Aayah za Qur-aan: Mwenye imani dhaifu hapendi kusoma Qur-aan, na akianza kuisoma ghafla hukumbuka kazi aliyosahau kuifanya, au akatafuta jambo la kumshughulisha ili asiendelee kuisoma, na hata anaposikia Qur-aan inasomwa hukosa utulivu wa nafsi na kutojishughulisha na kutafakari maana yake. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuambia: “Imeniotesha mvi (Surat) Huud na dada zake kabla ya uzee” Silsilat As-Swahiyhah. Aidha huwa mzito kufanya Dhikri na kumtaja Allaah, inaweza ikapita siku nzima hajamtaja Allaah na kumsifu nje ya Swalah, na Allaah Anawasifu watu wa aina hii kwa kusema: “Na wala hawamtaji Allaah isipokuwa kidogo.” 4: 142.

 

5.     Kutokuwa na wivu wa Dini:Mwenye imani dhaifu huwa hakasirishwi na madhilla yanayousibu Ummah, bali mara nyingine huwashangaa wale ambao wanakereka na dhulma dhidi y Uislamu, na kwa kutokuwa na imani kamili hushindwa kupata tafsiri ya wivu, na mara nyingine hutafsiri wivu, ukereketwa wa Uislamu kuwa ni jazbah, siasa kali au ujinga. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: “Linapotendeka ovu katika ardhi, yule anayelishuhudia kisha akalichukia anakuwa hayumo ndani ya ovu hilo, na yule ambaye hakulishuhudia ovu hilo lakini akaridhika nalo anakuwa ni sawa na alioshuhudia.” Abu Daawuud.

 

6.     Kupenda uongozi na kutojali Dhimma: Kupupia uongozi na kupenda cheo ni katika alama za udhaifu wa imani, mtu wa aina hii lengo lake kuu ni kufikia lengo lake, wakati mwengine hata kwa njia zisizokuwa sahihi. Anapofanya wema, anapofanya urafiki na mtu, anapowatembelea watu, anapoalika watu chakula, hata anapo tabasamu mbele za watu, basi kwa kiwango kikubwa hufanya hivyo kwa ajili ya kufikia uongozi au cheo.  Anasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Hakika yenu mtapupia uongozi, na utakuwa ni majuto (kwenu) siku ya Qiyaamah, ubora katika kunyonya na uovu katika kuacha ziwa.” Al-Bukhaariy.  Kwa maana mwanzo wa uongozi ni raha, lakini mwisho wake ni dhiki. Na katika Hadiyth nyingine, Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mkipenda niwafahamisheni kuhusu uongozi ni nini: mwanzo wake ni lawama, upili wake ni majuto, na utatu wake ni adhabu siku ya Qiyaamah isipokuwa kwa muadilifu.” At-Twabaraaniy. Waislamu wengi hivi leo alama hii tunayo, ukichunguza migogoro mingi iliyomo ndani ya Misikiti yetu, ndani ya Jumuiya na Taasisi zetu, sababu yake kubwa ni kugombea uongozi na cheo, leo Mashaykh zetu, wamekuwa mstari wa mbele katika kutafuta umaarufu na heshima kwa kuwakejeli wengine kuwa hawana elimu, hawana Sunnah, hawana kadhaa wa kadhaa, lakini ukichunguza kwa kina utakuta sababu kuu ni kupenda vyeo na kuheshimika, leo katika chaguzi za kamati za Misikiti yetu na Jumuiya zetu, watu wanafanya kampeni za uchaguzi, bali mtu anapita kwa waumini kuomba kura zao; hakika huu ni msiba mkubwa na kinyume kabisa na mafunzo ya Uislam.

7.     Ubakhili na Uchoyo: Ubakhili ni alama ya upungufu wa imani kama sio kutokuwa na imani kabisa. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:“Havikutani ubakhili na imani katika moyo wa mja hata siku moja.”An-Nasaaiy. Ubakhili unapoingilia dirishani basi imani hutokea mlangoni. Watu leo ni mabakhili kupita kiasi, hususan katika mambo ya Dini, bali mtu huona kama anapoteza mali yake anapoitoa katika shughuli za Dini, bali wengine ni mabakhili wa wakati, katika ratiba yake ya siku, hatoi hata saa moja ya kujitolea katika mambo ya Dini au Jumuiya yake. Wengine ni mabakhili wa elimu, ujuzi, na hata nasaha. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Anasema:“Jiepusheni na ubakhili, kwani hakika wameangamia waliokuwa kabla yenu kwa sababu ya ubakhili, (Shaytwaan) aliwaamuru ubakhili wakabakhilia, akawaamuru kukata undugu wakaukata, akawaamrisha kufanya maovu wakayafanya.”Abu Daawuud. Anasema Allaah: “Lo! nyinyi mnaitwa mtoe mali katika njia ya Allaah, kuna wengine katika nyie wanafanya ubakhili, basi afanyae ubakhili anafanya ubakhili huo kwa (kuidhuru) nafsi yake mwenyewe, Allaah ndio mkwasi na nyinyi ndio mafakiri…”47: 38.

 

Itaendelea inshaAllaah…

 

Advertisements

2 responses to “Udhaifu Wa Imani… Alama Zake, Sababu Na Matibabu Yake

  1. Assalam Alaykum, Tunamuomba ALLAH SUBHANAHUWATAALA atuepushe na alama za moyo uliokufa na azilainishe nyoyo zetu, HAKIKA YEYE HASHINDWI NA KITU CHOCHOTE YA RABI TUSAIDIE WAISLAM WOTE> AMEEEEEN.

  2. Asalam Alekum. JazakAllah kheir kwa kazi zenu nzuri.Allah awazidishi

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s