Kuja Kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)

Siku ya Jumatatu tarehe 12 mwezi wa Rabiul awwal (ipo khitilafu juu ya siku aliyozaliwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)), Mwenyezi Mungu aliwatunukia walimwengu wote zawadi kubwa sana kwa kuzaliwa kwa bwana wa viumbe vyote na kiongozi wao Muhammad bin ‘Abdullaah bin ‘Abdul Muttwalib Al-Haashimy kutoka katika kabila la ki Quraysh.

Alizaliwa akiwa yatima hana baba na alipotimia miaka sita mama yake akafariki na akachukuliwa na babu yake ‘Abdul Muttwalib, na miaka miwili baadaye babu yake akafariki na akachukuliwa na ammi yake Abu Twaalib.

Alipotimia miaka arubaini Mwenyezi Mungu alimpa utume ili awe mwenye kuleta bishara njema na mwenye kuonya, akausimamia ujumbe wake kama unavyostahiki kusimamiwa na akafikishi yale Mwenyezi Mungu alomuamrisha ayafikishe kwa ajili ya kuwatowa watu katika giza na kuwaingiza katika nuru. Wakubwa wa kabila lake wakamfanyia uadui na wakawatendea wafuasi wake kila aina ya udhia, wakamfuata makundi ya watu walioiuza dunia yao kwa ajili ya akhera, wakapigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na kwa nafsi zao, wakainusuru (dini ya) Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Mwenyezi Mungu Anasema;

“(Basi) wapewe (mali hayo) mafakiri wa Kimuhajiri ambao walifukuzwa katika nyumba zao na mali zao; (wakakhiari kuwacha hayo) kwa jili ya (kutafuta) fadhila za Mwenyezi Mungu na radhi (yake) na kuinusuru (dini ya) Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Basi hao ndio Waislamu wa kweli”.

Al Hashr – 8

 

Akaendelea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwalingania watu muda wa miaka kumi na tatu mpaka Mwenyezi Mungu alipomuamrisha kuhamia Madiynah, mji ambao Mwenyezi Mungu ameutia nuru kwa kumjaalia Mtume wake kuhamia huko. Wakahamia huko pia Maswahaba wake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na kuacha mali zao na watoto wao nyuma yao, yote hayo kwa ajili ya kutaka radhi za Mwenyezi Mungu.

 

Alipowasili Madiynah akapokewa vizuri na watu wa mji huo, waliomnusuru na kumsaidia. Wakawasaidia wale waliohama pamoja naye, wakagawana nao mali zao na nyumba zao na hata wake zao, kwani watu wa Madiynah wenye wake wawili au zaidi walikuwa wakiwaambia watu wa Makkah;

“Chagua mmoja kati ya wake zangu yule unayemtaka ili nimtaliki kisha nikuozeshe wewe”.

Mwenyezi Mungu Anasema;

“Na wale waliofanya maskani yaohapa (yaani Madiynah) na wakautakasa Uislamu (wao barabara) kabla ya kuja hao (Muhajir huko Madiynah) na wakawapenda hao waliohamia kwao, wala hawapati (hawaoni) dhiki nyoyoni mwao kwa hayo waliyopewa (hao Muhajiri), na wanawapendelea kuliko nafsi zao ingawa wenyewe wana hali ndogo. Na waepushwao na ubakhili wa nafsi zao hao ndio wenye kufaulu kweli kweli”.

Al Hashr –9

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akaendelea na da’awah yake nje ya mji wa Madiynah na hatimaye bara ya Arabu yote mpaka ilipofika siku ile tukufu ambayo Mwenyezi Mungu Alimfungulia Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) mji mtukufu wa Makkah (alipouteka mji wa Makkah) na watu wake wakaingia katika dini ya Kiislamu na baada ya hapo bara ya Arabu yote ikawa chini ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

 

Baada ya kuwalingania watu pamoja na kupigana jihadi muda upatao miaka ishirini na mitatu, ikamfikia qudra ya lazima kwa kila mtu inayosadikishwa na kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo;

“Na hakuwa Muhammad ila ni Mtume tu. Wamepita kabla yake Mitume (wengi kabisa),. Basi akifa au akiuawa ndiyo mtarudi nyuma (kwa visigino vyenu muwe makafiri kama zamani?) Na atakayerudi nyuma kwa visigino vyake hatamdhuru Mwenyezi Mungu chochote . Na Mwenyezi Mungu atawalipa wanaomshukuru”.

Aali ‘Imraan – 144

 

Dunia ilikuwa kama kwamba imeingiagiza totoro kutokana na tukio hili. Na kwa nini isiwe hivyo wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisema;

“Atakayekutwa kati yenu na msiba, basi akumbuke msiba wake kwangu (wa kifo changu), kwani huo ndio msiba mkubwa zaidi”.

Atw-Twabaqaat al-Kubraa na imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy.

Haukupata kutokea msiba mkubwa wakati wowote ule tokea iumbwe dunia kuliko msiba wa kifo cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Na huyu Bibi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) binti wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) wakati baba yake alipokuwa akijiwa na sakrati l mauti alikuwa akisema;

“Baba yangu! ameitikia mwito wa Mola wake, baba yangu! Pepo ya Firdausi makazi yake, baba yangu! kwa Jibril tunafikisha pole yake”.

Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) naye alisema;

“Siku ile Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipoingia mji wa Madiynah, kila kitu kilikuwa kikitowa mwangaza, ama siku ile aliyofariki kila kitu kiliingia giza, na tulipokuwa tukipangusa mikono yetu michanga baada ya kumzika tulihisi nyoyo zetu zimenyongeka (kwa sababu wahyi umeshakatika na hautoshuka tena baada yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)”.

 

Ibni Majah katika ‘Kitaabul Janaaiz – mlango wa ‘Wafaatun Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

Baada ya kifo cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), Abu Bakr alimwambia ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhum);

“Twende tukamtembelee Ummu Ayman”.

Walipowasili kwake, Ummu Ayman alilia sana, wakamuuliza;

“Kwa nini unalia hivyo wakati atakayopata Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa Mola wake ni bora zaidi?”

Akajibu;

“WaAllaahi ninalia si kwa sababu sielewi kuwa yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora zaidi kwa Mtume wake, isipokuwa kinachoniliza ni kukatika kwa wahyi kutoka mbinguni”.

Maneno hayo yaliwaliza sana Abu Bakr na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma)

Muslim

 

Na hivi ndivyo nafsi hii njema ilivyohamia kwa Mola wake

Advertisements

One response to “Kuja Kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)

  1. shukran kwako jamaa katika umat mohamed sww

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s