Hizbut Tahriyr Ni Nani, Wana Lengo Gani Na Je, Inafaa Kuwafuata?

Hizbut Tahriyr: Maana ya neno Hizbu ni Chama (umoja, walioungana), maana ya At-Tahriyr: kukifanya kitu kiwe huru, kukomboa. Hizbut Tahriyr ni chama cha kisiasa chenye mrengo wa Kiislamu, lengo lake kuu ni kurejesha mfumo wa Ukhalifa kwa kutegemea fikra na maono zaidi, katika kuleta mabadiliko hayo, tayari chama hicho kimeishatoa ijtihaadaat zake za kisharia ambazo nyingi miongoni mwa ijtihaadaat hizo zimepingwa vikali na wanachuoni wa Kiislamu wanaotambulika. Chama hiki kilianzishwa na Sheikh Taqiyyud Diyn An-Nabahaaniy mwaka 1909 – 1979 huko Palestina, alizaliwa katika kijiji cha mji wa Hayfaa, na masomo yake ya juu aliyachukulia katika chuo kikuu cha Al-Azhar na Dar Al-‘Uluum nchini Misri, na kisha akarudi Palestina na kuwa mwalimu na hatimaye akateuliwa kuwa Qaadhi katika maeneo tofauti nchini Palestina. Baada ya mwaka wa (nakbah) kushindwa kwa majeshi ya Kiarabu 1947-48 alihama yeye na familia yake katika mji wa Beirut, na hatimae kuteuliwa kuwa mjumbe katika Mahakama kuu ya Rufaa katika mji wa Quds, na kisha kuwa Mhadhiri katika Kitivo cha Uislamu Amman, Jordan. Mwaka 1952 aliasisi chama chake na akawa Raisi wa chama hicho, na shughuli zake kuu zikawa ni kuandika vitabu, makala, kusambaza vipeperushi kuandaa makongamano, warsha, mikutano ya kueneza sera na fikra ya chama hicho, na akawa ni mwenye kuhama hama baina ya Jordan, Syria na Lebanon, na hatimae alifariki na kuzikwa nchini Lebanon. Fikra Na ‘Aqiydah Ya Hizbut Tahriyr: Fikra na ‘Aqiydah ya Hizbut Tahriyr zinafanana na misingi mikuu ya Ahlus Sunnah Wal Jama’ah. Lengo lao kuu ni kurejesha maisha ya Kiislamu kwa kusimamisha Dola ya Ukhalifa katika nchi za Kiarabu kwanza, kisha kusimamisha Ukhalifa katika nchi za Kiislamu, na mwisho kabisa kufanya Da’wah katika nchi zisizokuwa za Kiislamu. Muasisi wa Hizbut Tahriyr alikuwa ameathiriwa kwa kiwango kikubwa na imani ya utaifa (Qawmiyyah) kama alivyobainisha hayo katika kitabu chake ((رسالة العرب (Ujumbe kwa Waarabu) na ndio maana akagawa watu katika misingi ya Uarabu, Uislamu, na Ukafiri. Muasisi wa chama hiki alikuwa na mahusiano ya karibu na Kundi la Ikhwaan Al-Muslimiyn (Muslim Brotherhood) la Jordan, lakini alitofautiana na kundi hilo katika muelekeo na vipaumbele (priorities) na kuamua kuanzisha chama chake. Kigezo kikuu cha Hizbu katika kufikia malengo yake hayo, ni kutumia mfumo wa fikra na ustaarabu wa Kiislamu katika kumjenga Muislamu katika shaqsiyah yake na kisha kuujenga Ummah wa Kiislamu, chama hutia mkazo mkubwa kwa wanachama wake kuhakikisha kuwa inawajenga katika mfumo wa kimwili zaidi kuliko kiroho. Malezi ya wanachama yanazingatia zaidi mwili na kupuuza mambo ya kiroho. Ni haramu kwa mwanaHizbu kuamini juu ya adhabu ya kaburi. Ni Haramu kuamini kuwa kuna Masiyh Ad-Dajjaal. Viongozi wa Hizbu wanaona kuwa suala la kuamrisha mema na kukataza maovu ni kikwazo cha kufikia malengo ya muda, na kazi hiyo ni jukumu la Dola ya Kiislamu na sio watu binafsi. Chama kina Katiba yake yenye vipengele 187 vya kusimamisha na kuendesha Dola ya Kiislamu. Fiqh Na Shari’ah: Katika vigezo vya kuzalisha hukmu za kisheria, hususan katika chimbuko la Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wanazuoni wa Hizbu wamejiwekea vigezo vigumu ambavyo kwa mujibu wa vigezo hivyo hujikuta wakitoa fatwa zenye utata mkubwa, kama vile kutokubali Hadiyth za Aahaad (Hadiyth zilizokuja katika mapokezi mamoja na si katika mapokezi ya wengi ‘Mutawaatir’) katika masuala ya ‘Aqiydah. Wanazuoni wa Chama hicho wametoa fatwa za ajabu kabisa katika mambo ya msingi kabisa katika Shari’ah za Kiislamu ambayo uharamu wake uko wazi, kama vile: Kuruhusu kuangalia picha za uchi. Kuruhusu kumbusu mwanamke asiyekuwa mahram yako wakati wanaposalimiana, kama zile salaam za wasiokuwa Waislam wanapokutana. Kujuzisha kwa Mwanamke kuvaa Wigi (Nywele za bandia) na Suruali. Kujuzisha kuacha kuswali na kufunga kwa wakazi wa North na South Pole. Wanajuzisha watu wanaoishi Ulaya kuchukua misaada katika serikali na kutokufanya kazi, wakidai kwamba maadam hakuna Khaliyfah basi kunakuwa hakuna mkataba na Makafiri au nchi na hivyo kutokufuata sheria zao na kukiuka taratibu zilizowekwa. Miaka ya 80 walikwenda viongozi wa Hizbu kumuona kiongozi wa Kishia wa Iran, Khomeini na kumpa bay’ah na kumuomba awakubali washirikiane nao katika kusimamisha Khilaafah, lakini Kiongozi huyo hakuwajibu chochote na mwisho waliachana naye na wakaifuta bay’ah yao kwake! Na masuala mengi madogo madogo. Masuala mengi kama haya wafuasi wadogo wadogo wa Hizbu ambao mara nyingi huwa ndio wenye hamasa na Jazba, hawayajui mengi katika haya, na hata wakitajiwa wanapinga kwa nguvu zote na kuhisi wanatuhumiwa. Inasikitisha wengi wao si wenye kutafuta elimu, wamegubikwa zaidi na hamasa na kufuatilizia tu mambo ya kisiasa na kupenda zaidi mjadala na malumbano na huwa mahodari sana wa kubishana na kila mmoja japo ataingia Hizbu siku chache na bila kuwa na elimu ya dini atasimama kwenye kiriri na kuhubiri na kupigania Khilaafah! HITIMISHO: Waasisi wa Hizbut Tahriyr, kama walivyokuwa waasisi wa makundi mengine ya Kiislamu kama Ikhwaan Al-Muslimiyn, waliasisi chama chao kutokana na uchungu waliokuwa nao juu ya hali ya Uislamu na Waislamu ulimwenguni. Lakini katika kuweka misingi ya kuyaendea malengo yao, walitumia vigezo vya fikra na uzoefu wa kisiasa zaidi ya vigezo vya ufahamu sahihi wa Qur-aan na Sunnah. Kama walivyokuwa Mu’utazilah katika kipindi cha nyuma, pamoja na juhudi kubwa waliyoifanya kupambana na falsafa na fikra za kizandiki, lakini waliingia katika kosa hili hili la kupima mambo kwa kutumia vigezo vya akili, mantiki, na falsafa, na kutafsiri mafunzo yote ambayo walikuwa wanayaona hayaendani na akili zao kwa mujibu wa ufahamu wao wa mazingira yao, jambo ambalo liliwaingiza katika uzandiki wa wazi kwa kukanusha mambo ambayo yana ushahidi sahihi wa Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hizbut Tahriyr ni chama cha kisiasa kimtazamo na kimuelekeo, na waasisi wa chama hiki wanakiri kupitia vitabu vyao kuwa ni chama cha kisiasa kabla ya kuwa chama cha Da’wah, hawaamini sana katika mihadhara na mawaidha kama inaweza kuleta mabadiliko, bali kwa juhudi za kisiasa na kubadili mifumo iliyopo. Kwa mwanahizbu kuanza juhudi zake katika nchi zisizokuwa za Kiarabu ni kwenye kinyume na malengo makuu na sera za Waasisi, bali mabadiliko yanabidi yaanzie katika nchi za Kiarabu, Ukhalifa unapopatikana katika nchi hizo, nchi zingine za Kiislamu zitashinikizwa kuingia katika mfumo wa Ukhalifa, na Dola ndio itasimamia baada ya hapo kazi ya kuamrisha mema na kukataza maovu. Kwa ujumla Hizbut Tahriyr kama chama kina makosa mengi na ya msingi, na kwa mfumo wake ni vigumu kupata mafanikio chanya kwa ajili ya Ummah, bali madhara yake yanaweza kuwa makubwa kwa mustakbali mzima wa Uislamu. Fikra yoyote inayopingana na mas-ala sahihi ya ‘Aqiydah yaliyothibiti, na kuachana na misingi ya mafunzo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kutawaliwa na matamanio ya nafsi na hisia na hamasa bila chimbiko lenye mashiko, haziwezi kuwa fikra za kufuatwa japo ziletwe na yeyote awaye. Hivyo, mwamko huo na harakati hizo, si rahisi kufanikiwa hadi kwanza zirejeshe ufahamu sahihi wa Uislam kama ulivyoletwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mfumo sahihi unaoweza kuleta faraja kwa Waislamu ni mfumo wa Ahlus Sunnah Wal Jama’ah kwa ufahamu wa As Salafus Swaalih, lakini kwa bahati mbaya mfumo huu bado haujafahamika vizuri na Waislamu waliokuwa wengi. Na Allaah Anajua zaidi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s