HAFSAH BINT ‘UMAR BIN AL- KHATTAAB

HAFSAH BINT ‘UMAR BIN AL- KHATTAAB 

UMMUL MUUMINIYN 

 

Hafsah ni mtoto wa ‘Umar ibnul Al -Khattaab na mama yake ni Zainab bint Madh’uun. Alizaliwa miaka mitano kabla Muhammad bin Abdillah kupewa utume mjini Makkah. Ni ndugu pamoja na sahaba maarufu Abdullah ibn ‘Umar Allah awawie radhi wote. 

Ndoa yake ya kwanza aliolewa na Khunais bin Hudhayfah bin Adiy ambae ni miongoni mwa waislamu wa mwanzo mwanzo. Khunais alikuwa miongoni mwa waislamu waliofanya Hijrah kwenda Habashah na alikuwa miongoni kwa waliofanya Hijrah kwenda Madina pamoja na mkewe Hafsah. Khunais walikuwa mwanajihadi shujaa kwani alipigana katika vita vya Badr na akashiriki katika vita vya Uhud ambapo alijeruhiwa vibaya. Alijaribu kutibiwa lakini aliporudi Madina alizidiwa na hatimae kufariki. Hafsah akabaki mjane.

 

Baada ya kumaliza eda, baba yake ‘Umar akaanza kumfikiria tena mtoto wake kuhusu kuolewa. Siku moja Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam alikuwa akizungumza faragha na Abu Bakr na kumgusia Hafsah na hali yake ya ujane. ‘Umar bila ya kujua kinachoendelea, aliwahi siku moja kuzungumza na Abu Bakr na kumuomba amuoe mtoto wake. Abubakr alinyamza kimya. ‘Umar alivunjika moyo, kwani alitaraji kupata jawabu kutoka kwa Abubakr. Kisha alikwenda kwa ‘Uthmaan kwa lengo hilo hilo ambaye naye karibuni alifiliwa na mke wake Ruqayyah, mtoto wa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam. ‘Uthmaan akaomba muda afikirie kabla ya kutoa uamuzi. Baada ya muda alirudi kwa ‘Umar na kumwambia hayuko tayari kumuoa Hafsah.‘Umar anasema kitendo cha Abubakr kunyamaza kimya hakikumfurahisha na pia kusikitishwa na ‘Uthmaan kutokuwa tayari kumuoa binti yake. 

Muda ukapita na ‘Umar aliwahi kwenda kwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam na kumfahamisha yaliyotokea. Mtume Salla ‘Allahu ‘Alayhi Wasallam akamposa na kumuoa. Kwani kuna riwaya inasema kwamba Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam alisema:

“Hafsah ataolewa na mtu bora kuliko ‘Uthmaan  na ‘Uthmaan ataoa mtu bora kuliko Hafsah”. 

Baada ya harusi kufanyika Abubakr aliwahi kukutana na‘Umar na akamwambia:

 “Nnajua ulihisi jambo wakati sikurudisha jawabu kuhusu (kumposa) Hafsah”.

 Akasema ‘Umar, “kweli”

Akasema Abubakr: “Nilifanya vile kwa sababu ya kuwahi kumsikia Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam akimtaja Hafsah; na sikuwa tayari kutoa siri za Mtume Salla ‘Allahu ‘Alayhi Wasallam. Na lau kwamba Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam asingemuoa basi ningelimuoa”     

 Baada ya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam kumuoa Hafsah; ‘Uthmaan alimuoa Ummu Kulthum binti mwengine wa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam.

Hafsah alikuwa ni mwingi wa kuwa na hamu ya kutafuta zaidi miongoni mwa elimu na maarifa aliyokuwa akipata kutoka kwa Mtume Salla ‘Allahu ‘Alayhi Wasallam. Mara nyingi likizungumzwa jambo hujaribu pia kutafuta faida zaidi kama siku moja Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam aliposema juu ya walioshuhudia  Badr na Hudaybiyah:

“ Nnatarajia hatoingizwa motoni inshaAllah miongoni mwa wote walioshuhudia Badr na Hudaybiyah

Hafsah akasema . “Lakini Allah Subhaanahu Wata’ala anasema katika Qur’aan Maryam/72

        وَإِن مِّنكُمْ إِلَّا وَارِدُهَا  

   Wala hapana yeyote katika nyinyi ila ni mwenye kuifikia 

Akikusudia kwamba kila mmoja miongoni mwetu anaweza kuingizwa motoni. Akamjibu Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam Maryam /73 

                 ثُمَّ نُنَجِّي الَّذِينَ اتَّقَوا وَّنَذَرُ الظَّالِمِينَ فِيهَا جِثِيًّا
 

Kisha tutawaokoa wale walio mchamungu; na tutawaacha madhaalimu humo wamepiga magoti

Ikumbukwe Hafsah si kwamba alikuwa akibishana na Mtume Salla ‘Allahu ‘Alayhi Wasallam bali alikuwa akitaka kupata ufafanuzi wa ziada ambayo aliupata kutoka kwa Mtume Salla ‘Allahu ‘Alayhi Wasallam. Hii ndiyo hima ya kutafuta elimu si kwa ajili ya kubishana bali kufaidika. 

Pia Hafsah ni miongoni mwa wapokezi wa Hadithi tofauti kutoka kwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wassallam. Inasemekana alipokea takriban hadithi zipatazo sitini kutoka kwa Mtume Salla ‘Allahu ‘Alayhi Wasallam na kupitia kwake tumeweza kujifunza mambo mengi katika dini yetu kama : 

       كان رسول الله صلى الله عليه وسلم إذا أوى إلى فراشه وضع يده اليمنى تحت                              خده وقال ( رب قني عذابك يوم تبعث عبادك ) ثلاث مرات

Alikuwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam anapolala kwenye kitanda chake huweka mkono wake wa kulia chini ya shavu lake na akiomba: “Ewe mola niepushe na adhabu yako siku watakapofufuliwa waja wako”  Akisema mara tatu.

Na hii ni miongoni mwa du’aa za kusoma wakati wa kulala. 

Hafsah pia ni miongoni mwa wake wa Mtume Salla ‘Allahu ‘Alayhi Wasallam ambao Malaika Jibriyl, ‘Alayhi Ssalaam, aliwashuhudia kwa kheri na kuwa na uchamungu. Jibriyl alisema: 

    ( إنها صوّامة ، قوّامة ، وهي زوجتك في الجنة ) رواه الحاكم ، و الطبراني ،                                                                               وحسنه الألباني    “Hakika ni mwanamke mwenye kupenda kuzitekeleza funga(za sunnah), mwenye kusimama usiku  kwa bidii naye atakuwa ni mkeo peponi”                    Haakim, Attabraaniy na Sh. Albani anasema ni Hasan. 

Kwani aliwahi kuachwa na baada ya ushauri wa Jibriyl,’Alayhi Ssalaam, Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam alimrudia. Hili ni fundisho muhimu la kujifunza katika historia ya kiislamu hasa waume wakati wanapotaka kuwaacha wake zao. 

Miongoni mwa alama za uaminifu na uchamungu ni pale alipokabidhiwa na khalifa Abubakr nakala ya kwanza kuandikwa ya Qur’aan kuihifadhi baada ya wengi miongoni mwa waliohifadhi kufariki. Alibaki nayo mpaka enzi za ukhalifa wa ‘Uthmaan bin Affaan.

 Uamuzi huu wa kupewa Hafsa uliangalia vigezo vingi kimojawapo kuwa ni miongoni mwa waliokuwa wakijua kusoma na kuandika vizuri baada ya kutafutiwa mwalimu wa kumsomesha na Mtume Salla ‘Allahu ‘Alayhi Wasallam – Bi Shifaa bint ‘Abdullah Adwiyah. 

Hata baada ya kufariki kwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam Hafsah aliendelea na ‘ibada za kukitihirisha kufunga funga za sunna pamoja na kukithirisha kusimama usiku kwa ajili ya ibada pamoja na kumtaja Allah Subhaanhu Wataala.

Ni miongoni mwa akinamama wa kiislamu waliojaaliwa elimu na maarifa ya dini. Ni miongoni mwa akinamama wa kuigwa na kupigiwa mfano katika uchamungu na kufanya ‘ibadah . Ni miongoni mwa wake wa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam ambao wamethibitishwa uchamungu wao na Malaika Jibriyl ‘Alayhi Ssalaam. Hiki ndicho kinatakiwa kiwe kigezo kwa akinamama cha kukiangalia na kuiga mfano wake. Amin

 Hafsah alifariki katika mwaka wa 41 Hijriyah na kabla ya kifo chake aliusia mali yake iliyokuwepo Ghabah itolewe sadaka kwa masikini na wasiojiweza. Hafsah hakujaaliwa kupata mtoto na Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s