Al-Israa Wal-Mi’iraaj (Sunnah- Siyrah)

بسم الله الرحمن الرحيم

“Ametakasika, Aliyemchukua mja Wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao Tumevibariki vilivyouzunguka, ili Tumwonyeshe baadhi ya Ishara Zetu. Hakika ni Mwenye Kusikia na Mwenye Kuona.” (Al-Israa 17: 1)

 

 

UTANGULIZI

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anaelezea Utukufu Wake, Ukubwa Wake na Uwezo Wake, kuwa Yeye ni Mweza wa kila kitu na Anafanya kila kitu Anachotaka kukifanya. Yeye pekee Ndiye Mungu wa kweli na Yeye pekee Yake Ndiye Mlezi (Muumba, Mtoaji wa Riziki na Mwenye kutoa ukimu wa kila kiumbe). Alimchukua mja Wake Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka Makkah na kumpeleka katika msikiti wa mbali huko Jerusalem katika usiku mmoja. (Kutoka Tafsiyr ya Ibn Kathiyr)

 

 

Miujiza Ya Mtume Wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)

Qur-aan

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipewa miujiza mingi na Mola wake. Muujiza wake mkubwa ni Kitabu cha Qur-aan, kitabu ambacho kiliteremshwa miaka 1400 iliyopita na hakuna hata mtu mmoja ambaye ameweza kubadilisha hata herufi moja au kuleta kitabu cha mfano wake. Allaah Amesema: “Hakika Sisi ndio Tulioteremsha Ukumbusho na hakika Sisi ndio Tutaoulinda” (Al-Hijr 15: 9).

 

Aayah hii ni changamoto dhidi kwa makafiri kuwaambia kitu kinachofanana na Qur-aan ambao walijaribu kufanya mifano ya Qur-aan wakawa wameshindwa vibaya sana. Vitabu vingine vya kutoka Kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) ni Taurati na Injili ambavyo viliharibiwa na kubadilishwa na ujumbe kubadilika ama kwa kuongeza maneno au kupunguza maneno na maana vile vile. Mwenyezi Mungu Amesema juu ya Qur-aan kuwa “Atailinda” na kweli Ameilinda na Ataendelea Kuilinda.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema, “Kila mtume aliyekuja kabla yangu alipewa muujiza na miujiza hiyo ilibakia kuwa miujiza wakati wa uhai wao hao mitume.: Mfano ‘Iysa (‘Alayhis-Salaam) alikuwa na muujiza wa kutibu watu wagonjwa na kufufua wafu Muusa (‘Alayhis-Salaam) alipewa fimbo ya miujiza na mambo mengine, nami nimepewa muujiza wa milele, Qur-aan itabakia kuwa muujiza hadi kusimama Qiyaamah. Hivyo natarajia kuwa wafuasi wangu watakuwa ni wengi katika idadi zaidi ya wafuasi wa Mitume wengine kwa kuwa muujiza wangu utabakia na utakuwepo hadi Siku ya Qiyaamah ambao ni Qur-aan. Kila anayekisoma Kitabu hiki hata kama ni mpagani basi yeye huvutika na kuona ukweli uliomo ndani yake na kuona hakuna aliyekiandika isipokuwa Bwana wa Mbingu na Ardhi.” (Swahiyh Al-Bukhaariy na Swahiyh Muslim)

 

 

Kupasuka Kwa Mwezi

Muujiza mwingine wa Mtume wa Mwenyezi Mungu ilikuwa ni kupasuka kwa mwezi. Anas anasema katika riwaya yake, kuwa watu wa Makkah walimtaka Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) awaonyeshe muujiza na akawaonesha kupasuka kwa mwezi. (Swahiyh Al-Bukhaariy, Juzuu ya 4 Namba 831)

 

 

Kutoka Maji Kutoka Vidole Vya Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)

Imepokewa kutoka kwa Jaabir ibn Abdullah akisema: “Nilikuwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na muda wa kuswali Swalah ya Al-‘Aswr ukafika. Tulikuwa hatuna maji isipokuwa maji kidogo tu ambayo yalikuwa ndani ya chombo ambayo yaliletwa kwa Mtume. Basi aliweka mkono wake ndani ya maji hayo na kutandaza vidole vyake na huku akisema, “Njooni Haraka watu wote ambao wanataka kutawadha Hii ni baraka kutoka kwa Allaah” Nikaona maji yakibubujika kutoka katika vidole vyake. Hivyo watu walitawadha na wengine wakawa wanakunywa maji hayo na mie nilitaka kunywa maji mengi kupita kiasi (kwa sababu nilijua kuwa ilikuwa ni baraka). Mpokeaji wa hadiyth hii kutoka kwa Jaabiri alisema kuwa nilimwuliza Jaabir Je, mlikuwa watu wangapi wakati huo? Akajibu, “Tulikuwa watu elfu moja na mia nne.”(Swahiyh Al-Bukhaariy Juzuu 7 namba 543 na Swahiyh Muslim Juzuu 4 namba 779)

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amepewa miujiza mingine mingi. Muujiza mwingine mkuu ni ule wa Israa na Mi’iraaj au “Safari ya Usiku” Makala hii ni kujaribu kuonesha faida zinazopatikana katika safari hii na mafunzo yanayopatikana katika muujiza huu mkubwa.

 

Tukio la Israa na Mi’iraaj lina hekima kubwa sana na mafunzo makubwa. Funzo lake kubwa ni kuwa mja hapaswi kukata tamaa, lazima awe daima anamtegemea Mola wale na atamletea faraja hata kama kutakuwa na mambo mazito yanamkabili. Zaidi ya hapo mwanadamu anapaswa kuwa daima karibu na Mola wake hasa wakati anapokuwa anakabiliwa na mambo mazito na vitendo vya kuhuzunisha au mikasa mizito, kwani matatizo hayo hupotea kama vile yalikuwa hayajatokea.

 

 

Mwaka wa Huzuni

Tukio la Israa na Mi’iraaj lilikuwa katika kipindi cha mwaka wa huzuni.  Mwaka huu ulipewa jina hilo kutokana na sababu zifuatazo:

 

1- Kifo cha ‘Ami ya Mtume, Abu Twaalib. Abu Twaalib alikuwa ni mlinzi na mlezi wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati Waislamu wakiwa Makkah na yeye alimkinga dhidi ya mashambulizi ya makafiri wa Makkah. Watu wa Makkah walipopinga ujumbe wa Muhammad kwa nguvu na kuanza kumshambulia Mtume na Waislamu, Abu Twaalib alikinga kifua chake na kumhami mtoto wa nduguye. Alisema, “Tunapenda kusaidia tunakubali ushauri wako na tunayakubali maneno yako. Hawa ni watu wa jamii yako ambao umewakusanya na mimi ni miongoni mwao, lakini mimi ni mwepesi kuliko wote kufanya kile ukitakacho. Fanya kila lile uliloamriwa kufanya. Nitakulinda na kukuhami, lakini siwezi kuiacha dini yangu” Abu Lahab akapayuka: “Wallaahi jambo hili ni jambo ovu Wewe lazima umkataze hayo ayafanyayo kabla ya watu wengine hawajamkanya”. Abu Twaalib akasema, Naapa nitaendelea kumlinda na kumhami katika maisha yangu yote”. (Ar-Rahiyqul-Makhtuum).

 

Ameeleza Al-‘Abbaas bin Abdul-Mutwalib (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa alimwambia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), “Hukuwa mwenye kumsaidia ‘Ami yako, Abu Twaalib, japo kuwa yeye alikuwa ni mtu mwenye kukuhami sana na alikuwa anachukizwa sana kwa mambo uliyokuwa unatendewa na Makureshi.” Mtume akasema, “Yuko katika moto mwepesi, kama si mimi angelikuwa kwenye moto wa tabaka la chini kabisa huko Jahanam.” (Swahiyh Al-Bukhaariy Juzuu 5 Namba 222); Hivyo Abu Twaalib licha ya kuwa kafiri alimuunga mkono Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa nguvu zake na mali zake dhidi ya makafiri. Wakati Abu Twaalib alipokuwa hai makafiri walikuwa hawawezi kumdhuru Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hata hivyo, kifo cha Abu Twaalib kilikuwa ni mwanya mwa makafiri wa kuendeleza vitimbi vyao dhidi ya Mtume pamoja na Waislamu kwa ujumla. Tabia yao ya ukatili ilimfanya Mtume aone maisha mjini Makkah ni magumu. Kutoa shahada kwa Maswahaba wa Mtume mjini Makkah ilikuwa ni njia ya kujitangazia uadui wa wazi wazi na wakawa wanapata madhila na kuadhibiwa vibaya. Kila aliyesilimu aliambiwa afanye moja kati ya mambo mawili: aritadi au aondoke hapo nchini au sivyo basi roho yake itafariki dunia; makafiri hawakutaka njia nyingine zaidi ya hiyo. Lakini Maswahaba  licha ya kuwa hiki kilikuwa ni kipindi kigumu sana na chenye taabu kubwa sana katika maisha yao kutokana na adhabu na madhila waliyoyapata, waliendelea kusimama imara juu ya imani ya Uislamu na walisonga mbele na Mtume wao katika msimamo huo. Kupanuka kwa Uislamu kuliwaudhi sana makafiri na wakajaribu kila njia ili kuzuia na kukinga Uislamu usiwepo katika nchi yao. Ulinganiaji wa dini hii ukawa mzito kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hata kuishi mjini Makkah ikawa ni hali ngumu sana kwake na kwa Waislamu.

 

2- Kifo cha mama wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) Ni miezi miwili tu baada ya kifo cha Abu Talib, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipata tatizo lingine zito lililomhusu yeye binafsi. Mke wake na Mama ya waumini, Bi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) alifariki. Mama huyu, mama wa Waumini Khadiyjah, alikuwa ni rehma kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala). Daima alikuwa na Mtume wakati akipata madhila na maudhi ya makureshi na alikuwa naye siku zote wakati wa mitihani mizito ilipokuwa inamwendea Mtume kutoka kwa mahasimu wake wa Kikureshi na walikuwa pamoja katika hali hiyo kwa muda wa miaka 25. Na kwa yote hayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ukaribu huo aliokuwa nao mama wa Waumini Khadiyjah alisikitika sana kwa kifo cha mkewe mpenzi na kuna wakati alisikika akisema juu ya bibi huyu,“Aliniamini wakati wengine hawakufanya hivyo, Alijiunga na Uislamu wakati watu walikuwa hawataki kufanya hivyo. Pia alinisaida na kuniliwaza mwenyewe na na kwa mali zake wakati kulikuwa hakuna hata mtu wa kuniunga mkono. Pia nilipata watoto kutoka kwake.’’(Musnad Ahmad 6/118).

 

Matukio haya mawili yalitokea mfululizo. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amefikia hali ya kubabaika namna gani awaongoze Waarabu wa Makkah, basi aliangalia upande wa Twaaif mji ambao kwa wakati huo ulikuwa unahitajia msaada na uongozi. Lakini hata huko pia hakupokelewa na hali hiyo kuongeza machungu moyoni mwake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hata akaona kipindi hicho kuwa ni “Mwaka wa Huzuni”.

 

Katikati ya huzuni zote hizo Allaah Alimchukua mja Wake katika muujiza mkubwa wa Israa na Mi’iraaj ili amwoneshe Aayah Zake na kumpatia msaada na himaya. Allaah Anasema, “Ili Tumwoneshe baadhi ya Ishara Zetu…”

 

Kwa muujiza wa Israa na Mi’iraaj , Mwenyezi Mungu Aliweka msingi kwa  waja Wake kuwa hata kama makafiri wangelifunga mlango wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Allaah Ndiye Mwenye Kumhami na  ndio Mlezi Wake na milango ya Peponi iko wazi kwa ajili ya Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hakuna nguvu ambayo inaweza kumteza au kumdhuru yule ambaye yuko chini ya ulinzi wa Mwenyezi Mungu. Israa na Mi’iraaj ilikuwa ni dalili ya kuonesha kufanikiwa kwa Da’wah ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ushindi wake juu ya maadui zake pamoja na kuwepo kwa matatizo na huzuni zote hizo.

 

 

Safari ya Israa

Lini kilikuwa Kipindi cha Israa na Mi’iraaj? Tarehe hasa ya tukio la Israa na Mi’iraaj haifahamiki kwa uhakika.  Ibn Kathiyr amenukuu kutoka kwa wanachuoni mbali mbali katika kitabu chake Al-Bidaayatu wan-Nihaayah (3/108) juu ya terehe ya tukio hilo. Wanachuoni wengi wanaona kuwa tarehe hiyo ilikuwa kati ya miezi 12 na 16 kabla ya Hijra yake kwenda Madiynah. Na wa zaidi ya hapo wamekhitilafiana juu ya siku na hata huo mwezi.

 

 

Kabla ya Safari

Malaika Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) alifungua kifua cha Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akatoa moyo wake na kuuosha kwa maji ya Zam Zam. Anasema Anas Bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu): “RasuluLlaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichukuliwa katika Israa na Mi’iraaj kutoka Msikiti Mtukufu wa (Makkah) Ka’abah. Watu watatu walimjia (ndotoni) akiwa amelala ndani ya Msikiti wa Makkah kabla Wahyi haujaletwa kwake. Mmoja wao akasema: “Ni yupi kati ya hawa watu?” Malaika wa kati akasema “Yule ambaye ni mbora kuliko wote” na Malaika wa Mwisho akasema, “Chukueni aliye mbora wao”. Mambo haya yalitokea katika usiku huo huo. Usiku huo hakuwaona, lakini aliwaona usiku mwingine ambapo tayari wahyi ulikuwa umeletwa kwake na alikuwa macho amelala lakini alikuwa hadhiri (Ni kawaida ya Mitume wote kulala macho wakati wako hadhiri). Wale Malaika hawakumsemesha bali walimbeba hadi wakamfikisha katika kisima cha Zam Zam. Miongoni mwao Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) alikuwa akiongoza na kuelekeza kifanyike nini. Alipasua  sehemu kati ya koo na kati ya kifua na  akatoa vyote vilivyokuwemo kifuani na kuviosha kwa maji ya Zam Zam kwa mikono yake mwenyewe na pia kusuuza sehemu za ndani za mwili na kisha kikaletwa chano cha dhahabu kikiwa na bakuli la dhahabu kililetwa ndani ya bakuli mkiwa mkajazwa  imani na busara. Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) akachukua vitu hivyo kutoka ndani ya bakuli na kuvijaza kifuani mwa Mtume kisha akachukua viungo vya Mtume pamoja na mishipa ya damu akavijaza kifuani kwa Mtume na kukifunga kifua”Swahiyh Al-Bukhaariy Juzuu 9 Namba 608, na Juzuu 5 Namba 227).

 

Israa maana yake ni safari ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yeye akiwa ni mwili wake na akili zake  na roho yake kutoka Ka’abah huko Makkah mpaka Msikiti wa Al-Aqswaa huko Quds (Jerusalem) akiwa amebebwa na mnyama wa ajabu mwenye kuvutia umbo lake  anayeitwa Buraaq na kisha safari ya kurejea kwake Makkah.

 

 

Al-Buraaq

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichukuliwa kutoka Msikiti wa Haram, Makkah mpaka Msikiti wa Al-Aqswaa mjini Quds juu ya mnyama aitwaye Al-Buraaq akiwa ameambatana na Malaika Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwelezea Al-Buraaq kuwa,“Nililetewa Al-Buraaq, mnyama mrefu wa umbo na mweupe, ni mkubwa kiasi zaidi ya punda  lakini ni mdogo kuliko nyumba, ambaye anapokwenda mbio hatua yake ni upeo wa macho yake. Nilimpanda mnyama huyo mpaka nikafika Msikiti wa Al-Aqswaa huko Al-Quds (Jerusalem). Hapo nilimfunga pale mahali ambapo Mitume wengine walikuwa wakifunga wanyama wao.” (Swahiyh Al-Bukhaariy na Swahiyh Muslim)

 

Anas Bin Maalik alisema, “Katika usiku ambao Mtume alipelekwa mbinguni, Al-Buraaq aliletwa kwake akiwa amefungwa vikuku na ana matandiko, lakini alileta ujeuri kidogo, na ndipo Jibriyl alipomwambia Al-Buraaq “Je unafanya haya kwa Muhammad? Hakuna mtu mtukufu aliyewahi kukupanda ambaye ni mtukufu zaidi ya huyu mbele ya Macho ya Allaah.” Kisha akatoa jasho.”  (At- Tirmidhiy na Musnad Ahmad)

 

 

Maana Ya Al-Buraaq Kwa Kiarabu Ni Mwale Unaotoka Katika Mwanga

Leo hii, Wanasayansi wanatuambia kuwa mwanga una mwendo kasi zaidi ya vitu vyote duniani. Huenda masafa ya maili 700 milioni kwa saa moja. Miaka 1400 iliyopita wakati ambapo kulikuwa hapajatokea utafiti na uvumbuzi palikuwa hakuna mtu ambaye aliweza hata kukisia mwendo kasi wa mwanga wala ukweli wake ukoje. Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walimwita mnyama huyo kama Al-Buraaq kwa msingi wa mwendo wake ulivyo na kasi kali.. Huu ni ukweli ambao unthibitisha ukweli wa Uislamu na ukweli wa Utume wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama Alivyosema Allaah ndani ya Qur-aan“Tutawaonyesha ishara Zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli.” (Fusswilat 41:53).

 

Hapo kale watu walipinga na kusema ‘mnyama huyo katokea wapi tena ambaye alimchukua Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka sehemu moja ya dunia mpaka nyingine na kisha kapita naye katika anga za mbingu na tena katika usiku mmoja?” Leo hii tunaona vipando ambavyo vimunda na binadamu, roketi na misali vikita maelfu ya maili kwa muda dakika chache tu. Iwapo mtu ambaye ni kiumbe cha Mwenyezi Mungu Muumba wa Ulimwengu, Je, Mwenyezi Mungu kwa nini asiumbe mnyama mwenye uwezo wa kukata masafa ya mamilioni ya maili kwa muda mfupi.

 

Kituo cha kwanza cha Safari – Al-Aqswaa:  Mtume alisema: “Kisha niliingia Msikiti wa Al-Aqswaa, nikaswali Raka’ah mbili” (Swahiyh Muslim)

Kuna riwaya nyingine ambazo zinaeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali na Mitume wengine hapo msikitini na yeye akiwa Imaam. Msikiti wa Al-Aqswaa umekuwa na sifa ya kuwa ni kituo cha Mitume wote. Toka siku ya Al-Khaliyl Ibraahiym (‘Alayhis-Salaam) hivyo Mitume wote walikusanyika hapo na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawa Imaam wao. Hii ni dalili ya nafasi kubwa aliyo nayo Muhammad ambaye ni Mtume wa mwisho miongoni mwa Mitume wengine (‘Alayhimus- Salaam). [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

Kisa cha Israa na Mi’iraaj kimeelezwa ndani ya Qur-aan (Al-Israa 17:1) Aayah inayofuatia inaeleza matendo ya aibu na makosa ya Mayahudi na kufuatia juu ya hayo makemeo makali ya Qur-aan. Mpangilio huo si kwa bahati tu, Al-Quds (Jerusalem) ilikuwa ni kituo cha kwanza cha safari hii ya Usiku na hapa kuna ujumbe ambao unaelekezwa kwa Mayahudi na kupewa ujumbe kuwa hadhi waliyokuwa nayo ya kuongoza dunia na binadamu kwa ujumla imetanguliwa. Utenguzi wa uongozi kwa mayahudi ulitokana na mabaya yao waliyokuwa wakiyafanya na yale ambayo wanaendelea kuyafanya.

 

Ujumbe huo unathibitisha wazi wazi kuwa uongozi huo umehamia kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) achukue uongozi wa makao makuu ya ‘Aqiydah ya Baba Ibraahiym na pia kuwa makao hayo sasa ni Makkah na Msikiti wa Mbali (Al-Aqswaa) huko Al-Quds (Jerusalem). Hivyo mamlaka hayo yalihamishwa kwenda kwenye taifa ambalo ni la Wacha Mungu na lenye utii kwa Allaah pamoja na Mtume ambaye amependelewa kubeba Qur-aan ambayo inaongoza watu kuelekea kwenye ukweli. [Ibara imechukuliwa kutoka katika kitabu Ar-Rahiyqul-Makhtuum].

 

 

Uchaguzi wa Asili (Fitwrah)

Vyombo viwili vya dhahabu vililetwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kimoja kikiwa kimejazwa maziwa na kingine kikiwa kimejazwa mvinyo (pombe). Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) alimwambia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) achague kinywaji kati ya hivyo vinywaji viwili. Mtume alichagua maziwa na akainua kile chombo na kuyanywa. Jibriyl alisema, “Umeongozwa katika fitwrah na umefikia daraja ya fitwrah. Kama ungelichagua mvinyo, watu wako wangelipotea.” (Swahiyh Al-Bukhaariy Juzuu 6 Namba 232)

 

[Neno fitwrah lina maana ya silika asili ambayo imo kwa kila mtoto anapozaliwa, silika hiyo inamtambua Mwenyezi Mungu Allaah; kama silika hiyo haikufisidiwa humpeleka mja katika Imani ya Tawhiyd ya Allaah.]

 

Imaam An-Nawawiy alisema kuwa kauli ya Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) kwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), “Umechagua fitwrah” maana yake Mtume alikuwa amechagua dini ya Islam, yaani “Umechagua nembo ya Islaam na Istiqaamah (kuwa imara katika Njia Iliyonyooka). Maziwa yalikuwa ni alama tu kwa sababu ni rahisi kuyanywa wakati mvinyo ni “mama wa maasi na maovu” na chanzo cha matendo ya kikatili”.

 

Kwa lugha nyepesi ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliletewa vitu viwili; kimoja kinawakilisha matendo mema na kingine kinawakilisha matendo maovu na viliwekwa mbele ye Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kwa silika akachagua kile kilicho kizuri. Kwa leo hii mtu akiacha fitwrah na kuanza kutafuta vitu vinginevyo anaonekana jinsi anavyohangaika baada ya kuacha njia ambayo amewekewa na Mola wake. Ni wajibu wa binadamu kushikamana na Njia ambaye ameamrishwa na Allaah kwa sababu, “Na atakayejiepusha na mawaidha Yangu, basi ya kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Qiyaamah Tutamfufua hali akiwa kipofu” (Twahaa 20:124)

 

“Na aliyekuwa hapa kipofu, basi atakuwa kipofu Akhera, na atakuwa aliyeipoteza zaidi Njia” (Al-Israa 17:72)

 

Mi’iraaj ni hali iliyomfikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kupaa mbinguni kutoka Msikiti wa Al-Aqswaa na kwenda katika Mbingu na hata akawa amekutana na Mwenyezi Mungu.

 

Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) alikuwa naye katika msafara huo wa kupaa. Ibn Kathiyr aliandika katika kitabu chake cha Al-Bidaayatu wan-Nihaayah:“Safari ya kupaa haikuwa kwa kutumia Al-Buraaq kwa sababu alikuwa amefungiwa katika mlango wa Baytul-Maqdis, akisubiri Mtume akirejea kutoka mbinguni ili ampeleke Makkah.”

 

Baada ya ziara ya Masjid Al Al-Aqswaa, Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) na Mtume walianza safari ya kwenda mbinguni. Kila alipofika kwenye mbingu alibisha hodi na aliulizwa na walinzi wa mbingu hiyo, “Wewe nani?” na alipojibu kuwa ni “Jibriyl!” aliuliulizwa tena, “Nani umefuatana naye?” Alisema “Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)” Na aliulizwa tena, “Je ameitwa?” Na Jibriyl alijibu, Naam, Hakika ameitwa!” Na ndipo Malaika walisema “Marhaba, Anakaribishwa, Safari yake ni Njema kabisa.” Milango ilifunguliwa na wakamwona Aadam (‘Alayhis-Salaam). Jibriyl alisema akimwambia Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Huyu ni baba yako Aadam (‘Alayhis-Salaam). Mpe heshima zake kwa salaam”. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimsalimu na Aadam aliitikia na akasema, “Unakaribishwa Ewe Mwanangu Mtume Mtukufu” na akamwombea du’aa njema.

 

Kisha walipanda mbingu ya pili na sawa kama hapo awali Jibriyl alibisha hodi na kuwaomba walinzi kufungua milango ya Mbingu na wakamuuliza maswali kama yale aliyoulizwa hapo mbingu ya kwanza. Hali ya namna hiyo iliendelea hadi kufika mbingu ya saba. Hatima milango ilifunguliwa  na wakawa wamekaribishwa  kwa kauli ya “Marhaba, Anakaribishwa, Safari yake ni Njema kabisa.”

 

Katika Mbingu ya pili Mtume alimwona ‘Iysa bin Maryam (‘Alayhimas-Salaam) na Yahya ibn Zakariyah (‘Alayhimas-Salaam) mtu na binamu yake. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema, “Nilikutana na ‘Iysa bin Maryam. Alikuwa na umbo la wastani na uso wake ni mwekundu kama vile katoka kuoga…” (Swahiyh Al-Bukhaariy Juzuu 4 Namba 647) Jibriyl alisema, “Hawa ni Yahya bin Zakariyah na ‘Iysa (‘Alayhimus Salaam) wasalimu”, na Mtume aliwasalimu na wote wawili walijibu salamu zake na kusema “Unakaribishwa Ewe ndugu yetu Mtume Mtukufu” na kisha wakamwombea dua njema.

 

Baada ya hapo walipanda Mbingu ya Tatu ambako walimkuta Yuusuf (‘Alayhis-Salaam) ambaye amejaliwa uzuri wa sura wa nusu ya dunia. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimsalimu naye akajibu salamu hiyo na akamkaribisha na akaondoka nao wakaenda Mbingu ya Nne pamoja. Milango ya Mbingu ya Nne ilifunguliwa na Idriys (‘Alayhis-Salaam) alikuwa hapo. Qur-aan inasema juu yake: “Na mtaje katika Kitabu Idriys. Hakika yeye alikuwa mkweli Nabii.  Na Tulimuinua daraja ya juu”. (Maryam 19: 56-57).

 

Idriys (‘Alayhis-Salaam) alimkaribisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wakasalimiana. Kisha Idriys aliondoka nao wakaenda Mbingu ya Tano ambako walimkuta Haaruun (‘Alayhis-Salaam). Mtume Haaruun (‘Alayhis-Salaam) aliwapokea na akajibu salamu zao na kumwombea dua njema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Kisha Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipelekwa Mbingu ya Sita ambako alimkuta Muusa (‘Alayhis-Salaam). Mtume anamsema, “Nilikuta na Muusa (‘Alayhis-Salaam) nilipokwenda Mi’iraaj. Alikuwa ni mtu mrefu akiwa na nywele ndefu kama vile ni mtu wa kabila la Shanu (Swahiyh Al-Bukhaariy Juzuu 4 Namba 647).

Muusa (‘Alayhis-Salaam) alimkaribisha Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Jibriyl (‘Alayhis-Salaam), na wakasalimiana na walipoondoka kuendelea na safari yao, Muusa (‘Alayhis-Salaam) alilia. Aliulizwa kwa nini analia basi Muusa (‘Alayhis-Salaam) alijibu, “Nalia kwa sababu amepelekwa Mtume duniani baada yangu, kijana ambaye wafuasi wake wataingia peponi kwa makundi makundi zaidi ya watu wangu”.

 

Kisha waliendelea na safari yao kuelekea Mbingu ya Saba na huko wakamkuta Ibarahiym (‘Alayhis-Salaam) akiwa ameegemea Baytul-Ma’amuur (Nyumba ambayo inatembelewa mara kwa mara). Ndani ya nyumba hii kila siku wanaingia malaika 70,000 na wala hawarudi tena … na Mtume alisema, “Nilimwona Ibraahiym (‘Alayhis-Salaam) ambaye mimi nafanana naye sana kuliko watoto wake wote” [Swahiyh Al-Bukhaariy Juzuu 4 Namba 647]. Ibraahiym alimkaribisha Muhammad na wakasalimiana na Ibraahiym (‘Alayhis-Salaam) akamwombea dua njema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) [Angalia maelezo ya Swahiyh Al-Bukhaariy Juzuu 5 Namba 227 na Swahiyh Muslim]

 

Ameeleza ‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu): Mtume alisema, “Ndani ya usiku wa Mi’iraaj nilikutana na Ibraahiym (‘Alayhis-Salaam) ambaye aliniambia, “Muhammad wapelekee Salaam zangu watu wako na waambie kuwa Pepo ni uwanda mpana ambao umeenea udongo safi, maji safi na miti yake hutoa sauti, “Subhaana Allaah, AlhamduliLaah La ilaha illa Allaah Allaahu Akbar.” [At-Tirmidhiy namba 1445)

 

 

Kituo Cha Mwisho Cha Safari- Sidratul-Muntahaa

Amesema ‘Abdullaah bin Mas’uud,“Wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipochukuliwa safari yake kwenda Mbinguni alifikishwa mpaka Sidratul-Muntahaa ambapo kila kitu kinachopanda kutoka ardhini hukomea na na kile kinachoshuka kutoka juu hukomea hapo…” (Muslim 329)

 

RasuluLlaah akasema, “Kisha nilichukuliwa hadi Sidratul-Muntahaa mti ambao majani yake ni kama masikio ya tembo na matunda yake makubwa kama mitungi. Na mti huu ulipogubikwa na amri za Mwenyezi Mungu, basi ulibadilika kuwa katika hali ambayo hakuna kiumbe ambaye anaweza kumsabihi Allaah kwa uzuri wake.” (Muslim)

 

Kisha katika riwaya nyingine: “Kisha nilipandishwa Mbinguni hadi kufikia Sidratul-Muntahaa. Matunda yake yalikuwa makubwa kama magudulia ya Hajr (sehemu ambayo ni karibu na Madiynah) na majani yake yalikuwa makubwa kama masikio ya tembo. Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) akasema, “Huu ni mkunazi wa mbali kabisa” Kulikuwa na mito minne karibu yake miwili ikiwa haionekani na miwili ikiwa wazi inaonekana. Nikauliza, “Hii mito miwili ni mito gani? Ewe Jibriyl” Basi akajibu, “Ama kwa mito miwili isiyoonekana ni mito miwili ya Peponi na mito miwili inayoonekana  ni mto wa Naili (Nile) na Furati (Euphrates).”

 

Hii hadiyth haina maana kuwa mito hiyo miwili inayoonekana kuwa asili yake ni Peponi, lakini ni kuonyesha tu mahali ambapo atakuwepo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na watu daima watabakia wenye kushikamana na Uislamu na kurithishana kizazi kimoja baada ya kingine. (Ar-Rahiyqul- Makhtuum).

 

RasuluLlaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pia alisema, “Jibriyl alinipandisha mbinguni hadi tukafika Sidratul-Muntahaa (mkunazi ambao una mpaka wa mwisho) ambao ulikuwa umepamba kwa rangi ambazo haziwezi kuelezeka. Kisha niliruhusiwa kuingia Pepopni ambamo nilikuta mahema (madogo madogo) au kuta ambazo zimejengwa kwa lulu na ardhi yake ilikuwa ni ya miski.” [Al-Bukhaariy Juzuu 1 Namba 345].

 

Wakati nilikuwa natembea humo peponi (katika usiku wa Mi’iraaj) niliona mto na katika kingo zake kulikuwa na vijihema ambavyo vimejengwa kwa kutumia lulu zenye uwazi katikati. Niliuliza, ‘Nini kile Ewe Jibriyl?’ Akasema huo ndio mto wa Kawthar ambao Mola wako amekupa wewe. Basi harufu iliyotoka humo au kwenye matope ilikuwa ni miski. (Mmoja wa wapokeaji wa riwaya hii, Hudba hana hakina ilikuwa imetumika ibara gani.) [Swahiyh Al-Bukhaariy Juzuu 8 Namba 583]

 

“Katika usiku wa Mi’iraaj huko mbinguni pia nilimwona Maalik mlinzi wa Milango ya Motoni na Ad-Dajjaal miongoni mwa miujiza ambayo Mwenyezi Mungu Alinionesha huko.”

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kisha akasoma, “Hakika Sisi Tulikwishampa Muusa Kitabu”. Hivyo usiwe na mashaka juu ya kukutana na Muusa (‘Alayhis-Salaam) huko mbinguni katika usiku wa Mi’iraaj (Al-Bukhaariy Juzuu 4 Namba 462]

 

Na kwa riwaya nyingine Anas bin Maalik amesema, “RasuluLlaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema, “Katika usiku wa Mi’iraaj nilipopandishwa kupelekwa Mbinguni nilipita karibu na watu ambao walikuwa wana makucha ya shaba na walikuwa wakijiparura nyuso zao na vifua vyao. Nilisema; Hawa ni nani ewe Jibriyl? Alijibu na kusema kuwa: Hawa ni wale watu waliokuwa na tabia ya kusengenya na kuwazulia watu maneno machafu na kuharibu heshima za watu” [Sunan Abu Daawuud namba 4860]

 

Na katika riwaya nyingine, Abu Hurayrah anasema: RasuluLlah alisema: “Katika usiku wa Mi’iraaj nilipopelekwa Mbinguni niliona watu ambao matumbo yao yalikuwa makubwa kama nyumba na ndani yake kuna majoka ambayo yalionekana nje ya matumbo yao. Niliuliza kuwa walikuwa kina nani, na Jibriyl alinijibu kuwa wao walikuwa wale watu waliokuwa wakila mali ya riba”. [Musnad Ahmad, Ibn Maajah na At-Tirmidhiy namba 2828]

 

Kasema Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu):  “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Usiku wa Mi’iraaj nilipopelekwa Mbinguni niliwakuta watu na midomo yao ikichanwa na mikasi ya moto. Nikamuliza Jibriyl ni nani hao na akasema walikuwa ni wahubiri miongoni mwa wafuasi wangu, ambao walisema ambayo wao hawakuyafanya” [At-Tirmidhiy (ghariyb) Namba 4801]

 

Buraydah bin Al-Haasib (Radhiya Allaahu ‘anhu) alieleza jinsi siku moja asubuhi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyomwita Bilaal na kusema, “Umefanya nini mpaka ukaingia Peponi kabla yangu? Sikupata kuingia peponi pasina kusikia mchakacho wako ukiwa mbele yangu. Bilaal akajibu, ‘Sijapata kuadhini ila baada yake kuswali rakaa mbili. Na sijapata kutenguka wudhuu ila nilitawadha papo hapo na kujiona kuwa nina deni kwa Mwenyezi Mungu la rakaa mbili. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, “Ni kwa sababu hizo,” [At-Tirmidhiy namba 326].

 

Na Jaabir bin ‘Abdullaah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema, “Nilijiona naingia Peponi na mara nikamwona bi Ar-Rumayswah, mke wa Abu Twalhah. Nilisikia hatua za mtu. Nikauliza, “Wewe nani?”. Mtu mmoja akajibu: “Ni Bilaal” kisha nikaona kasri na mwanamke akiwa amekaa katika ukumbi wake. Nikauliza, “Kasri la nani hili?” Basi kuna mtu alijibu, “Hilo la ‘Umar” Nikatamani kuingia ili nione ndani kukoje, lakini nilikumbuka jinsi ‘Umar alivyo na wivu (ghiyrah) basi sikuingia” Mara ‘Umar akadakiza “Fidaka Abiy wa Umiy, Yaa RasulaLlaah! Nitathubutu namna gani mimi kudhania kuwa umenikosea wewe kwa kuingia kwangu?” [Al-Bukhaariy Juzuu 5 Namba 28]

 

Kutokana na Hadiyth hizi tunaona jinsi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa mtu mwenye kulea watu wake na kuwafundisha mambo kwa hekima. Alipowafundisha tabia njema haikuishia bali yeye aliyafanya hayo kwa mifano ya wazi wazi kabisa. Alipata kusema, “Kama mtu atachungulia katika nyumba ya mtu bila rukhsa ya mwenyewe na huyo mwenye nyumba akachokora jicho lake, kutakuwa hakuna tatizo wala hilo jicho halitalipwa fidia”. [Sunan Abu Daawuud namba 5153]. Kwa sababu yule anayechungulia katika nyumba za watu amefanya wizi kwa kuingilia siri za watu na hifadhi zao na hivyo Allaah Ametoa hukumu kali kwa kosa wizi. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Mkono wa mwizi unapaswa kukatwa hata kama kwa wizi wa robo dinaar” [Al-Bukhaariy Juzuu 8 Namba 781]

 

 

Mtume Anakutana Na Allaah – Je, Mtume Alipata Kumwona  Mola Wake?

“Kisha akakaribia na akateremka. Akawa kama baina ya mipinde miwili au zaidi. Akamfunulia mja Wake, Alichomfunulia. Moyo haukusema uongo uliyoyaona. Je, Mnabishana naye kwa aliyoyaona? Na akamwona mara nyingine. Penye Mkunazi wa Mwisho. Karibu yake ndipo ipo Bustani inayokaliwa. Kilipo ufuniko huo Mkunazi hicho kilichofunika. Jicho halikuhangaika wala halikuruka mpaka. Kwa yakini aliona katika Ishara  kubwa kabisa za Mola wake.  [Angalia Al-Bukhaariy Juzuu 9 Namba 609]

 

Waislamu wa mwanzo walitofautiana juu ya kwamba Mtume alimwona Mola wake kwa jicho lake au hapana.

 

Mama wa Waumini ‘‘Aaishah, Abu Hurayrah na Ibn Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhum) wanakataa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwona Mwenyezi Mungu kwa macho yake. Kuna riwaya kupitia kwa Ibn Abi Haatim kwamba Ibn Mas’uud alieleza Aayah zilizotajwa hapo juu, kwamba, “Mtume alimuona Jibriyl katika umbo lake halisi mara mbili. Na Mara Jibriyl alipokuwa katika umbo lake halisi basi alifunika anga yote kwa mwili wake. Kwa mara ya pili Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwona katika umbo lake halisi ni wakati wa safari yao ya kwenda Mbinguni. Na hiyo ndiyo maana ya maneno, “Naye Yuko juu kabisa ya upeo wa macho” (Tafsiyr Ibn Kathiyr) Hivyo aya hii inaonesha kuwa Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) alijongea  na kuwa  karibu na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) (Fat-hul-Baariy  ukurasa 263, 264  ya Juzuu 17)

 

Amesimulia Masruuq (Radhiya Allaahu ‘anhu), “Nilimwuliza mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) “Ewe mama wa Waumini, Je Mtume alipata kumwona Mola wake?, mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) akasema, “Hicho ulichokisema kinafanya mwili wangu kusisimka na nywele kujivuta. Jua kuwa iwapo mtu atakwambia kitu katika hivi vitatu vifuatavyo ni mwongo: “Mtu akikwambia kuwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwona Mola wake, ni mwongo huyo” Na kisha mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) akasoma aya, “Macho hayamfikilii bali Yeye Anayafikilia macho. Naye ni Mjuzi, Mwenye khabari,” (Al-An’aam 6:103)

 

“Na haikuwa kwa mwanadamu kwamba Mwenyezi Mungu Amsemeze ila kwa wahyu (ufunuo) au kwa nyuma ya pazia.”  [Ash-Shuura 42:51].

Jambo la pili kama mtu atakwambia nini kitatokea kesho, ni mwongo” na Kisha akasoma Aayah, “…Na haijui nafsi yo yote nini itachuma kesho…”  [Luqman 31:34] na pia akaongezea jambo la tatu kwa kusema, “Ye yote atakayekuambia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alificha baadhi ya wahyu alioletewa na Mwenyezi Mungu kutangaza, ni mwongo na akasoma aya, “Ewe Mtume! Fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi…”  [Al-Maaidah 5:67]. Kisha mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliendelea kusema, Lakini Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwona Jibriyl (Alayhis-Salaam) katika umbo lake halisi mara mbili. [Al-Bukhaariy Juzuu 6 Namba 378].

 

Kwa upande mwingine Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alisema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona Mwenyezi Mungu, na akasema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwoma Mola wake mara mbili. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Al-Haafidh, Ibn Hajar alisema, “Maelezo ya Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) yamekuja katika hali ya kutodhibitiwa (hayaelezi kama Mtume alimuona Mola wake kwa macho yake au vipi) wakati kauli za mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) na wenziwe zimedhibitiwa kwa kusema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakumwona Mwenyezi Mungu “Kwa macho yake”. Tunaweza kuunganisha kauli hizo mbili kwa kusema mama wa Waumini ‘Aishah (Radhiya Allaahu ‘anha)  alikataa mwono “Kwa macho yake” na kauli ya Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa ni kamuona kiroho”.  [Fat-hul-Baariy 8/608]

 

Pili, kauli hizo mbili, ya mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) na ya Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma), kwa njia nyingine kuwa kauli ya Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alisema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona Mola wake wakati akiwa katika usingizi, jambo ambalo ni ndoto ya kweli na isiyokuwa alimwona Siku ya Mi’iraaj wakati kauli ya mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) inakataa kuwa Mtume hakumuona Mola wake wakati yeye akiwa macho, lakini kauli hiyo haikatazi kuwa  Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwona Mola wake akiwa usingizini. Alichokana hapa ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakumuona Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa macho yake meupe, akiwa macho.

 

Wale ambao wanao msimamo kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwona Mola wake kwa macho yake meupe wanaleta Hadiyth Dhaifu. Hakuna Hadiyth Sahihi ambayo inaeleza ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwona Mola wake kwa macho yake akiwa macho. Wenye msimamo huo wanaleta Hadiyth ya At-Tirmidhiy ambayo Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) anasema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwona Mola wake. Ikrimah alimuuliza: “Vipi Aayah ambayo inasema, “Macho hayamfikilii bali Yeye anayafikilia macho.”. Alijibu, kuwa ni wakati tu Mwenyezi Mungu amezungukwa na Nuru, lakini Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwona Mola wake mara mbili.  “Hadiyth hii ni dhaifu”

 

Kwa hali hiyo kwa namna jinsi ilivyo hakuna mgongano wa kauli na Mwenyezi Mungu Anajua zaidi. [Sharh ya Uswuul Al-I’itiqaad cha Lailakiy, 93/512, As-Sunnah 1/181 na Swifat Al-Maqdisiy ukurasa 109-111]

 

Zawadi Ya Mi’iraaj

‘Abdullaah bin Mas’uud alisema,“RasuluLlaah alipewa vitu vitatu: alipewa Swalah tano, alipewa aya ya kumalizia Surah ya Al-Baqarah na kusamehewa kwa madhambi ya wale watu ambao hawamshirikishi Mwenyezi Mungu miongoni mwa umati wake.” [Muslim Namba 329]

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Allaah Alinipa ufunuo na Akasema kuwa Ummah wangu wanawajibika kuswali Swalah 50 kila siku; usiku na mchana. Nilishuka kwenda kwenye Mbingu ya Muusa (‘Alayhis-Salaam) akaniluza, “Lipi Mola wako Amekupatia kwa ajili ya umati wako?, Nikasema, “Swalah Khamsini”  Akasema Rejea kwa Mola wako na omba Akupunguzie  katika idadi hiyo ya Swalah, maana watu wako hawawezi kubeba mzigo huo mzito. Kama vile nilivyotiwa katika mtihani na Wana wa Israeli, na nikawajaribu nikawaona kuwa walikuwa dhaifu sana na hawawezi kubeba mzigo kama huo.” Hivyo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimgeukia Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) kama vile akitaka kupata ushauri wake juu ya hilo. Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) akasema, “Ndiyo, sawa, kama unataka hivyo”. Na wakarejea tena juu kwa Mwenyezi Mungu.” [Al-Bukhaariy Juzuu 9 Namba 608]

 

Kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema,“Nilirejea kwa Mola wangu na kusema, “Ewe Mola wangu, Fanya vitu viwe vyepesi kwa ajili ya Ummah wangu. Mwenyezi Mungu Alipunguza  idadi ya Swalah 50 na kuwa tano kwa ajili yangu. Nilishuka chini nikaenda kwa Muusa (‘Alayhis-Salaam) ambaye alisema, “Hakika watu wako hawataweza kubeba mzigo huu mzito. Rejea kwa Mola wako umwombe afanye wepesi wa hilo, Ewe Muhammad”. Mimi nilijaribu kuwalingania Ummah wangu Wana Israeli ili wafanye kidogo zaidi ya hayo, lakini hawakuweza kuyafanya hayo bali waliishia kukata tamaa.” [Al-Bukhaariy, Juzuu 9 Namba 608]. Basi nikawa natangatanga kati ya Mbingu ya Muusa na kwa Mola wangu mwisho Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Akasema: “Kuna Swalah tano kila siku, usiku na mchana Ewe Muhammad. Kila Swalah imebeba uzito wa Swalah kumi, na hivyo hizo ni Khamsini vile vile. Mtu yeyote anayetia nia ya kufanya jambo zuri na asipolifanya basi atapata thawabu kwa hilo, na kama atalifanya hilo tendo, basi itaandikwa thawabu kumi kwa hilo. Wakati ambapo mtu aliyenuia kufanya uovu na akaacha kuufanya haitasajiliwa hiyo na kama atafanya uovu huo basi utasajiliwa uovu mmoja tu. Hapo nikashuka kwa Muusa (‘Alayhis-Salaam) na kumwambia hayo, Muusa akasema,” Nenda kwa Mola wako ili afanye mambo yawe mepesi zaidi”. Juu ya kauli hiyo Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, “Nimekuwa nikienda kwa Mola wangu mara kwa mara hadi naona aibu kusimama mbele yake. (Muslim). Juu ya hilo Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) akasema,”Kwa jina la Mwenyezi Mungu! Shuka sasa! Kisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaamka akiwa ndani ya Msikiti Mtukufu wa Makkah.” (Swahiyh Al-Bukhaariy Juzuu 9 Namba 608) na pia ndani ya maelezo ya Al-Bukhaariy kuna maelezo zaidi kuwa, …Nilipoondoka nilisikia sauti “Nimetoa amri yangu na kisha nimewapunguzia uzito Waja Wangu”.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ameitukuza Swalah na kuipa daraja kubwa sana kwa kuifaradhisha katika usiku wa Mi’iraaj Amri zote zingine zililetwa na Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) ardhini kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Swalah ilifaradhishwa baada ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuitwa kwenda Mbinguni na mawasiliano yalikuwa ni moja kwa moja kutoka kwa Mola hadi kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Aya nyingi za Qur-aan na Hadiyth nyingi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zinashuhudilia utukufu na umuhimu wa Swalah.

 

Ibn Hajar anaandika katika sharh yake ya Al-Bukhaariy (1/460), “Hekima ya kufaradhishwa Swalah wakati wa Mi’iraaj ni kuwa hapo ndipo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipopata utukufu kamili kwa nje na ndani ya mwili wake. Alikoshwa kwa maji ya Zam Zam na kisha akanyunyuziwa na Iymaan na hekima. Kwa kuwa Swalah imetanguliwa na wudhuu, ilikuwa hasa mahali pake maamrisho ya Swalah yaletwe akiwa katika hali hiyo yaani baada ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutakaswa na kusafishwa.”

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema: “…Na Mkizihesabu neema za mwenyezi Mungu hamwezi kuzidhibiti,” Kupunguzwa kwa idadi ya Swalah ni neema kutoka kwa Mwenyezi mungu na kisha Allaah Amesema: “Ni wachache katika waja wangu wanao shukuru.” [Saba-a 34:13] na “Hakika mwanadamu ni mtovu wa fadhila kwa Mola Wake Mlezi” [Al-‘Adiyaat 100:6]. Je, kuna neema gani tukufu ziaidi ya hii kuwa  Swalah ambazo zilikuwa ni Khamsini zimepunguzwa na kuwa tano kwa siku, usiku na mchana  na kisha malipo ya hizo Swalah tano ni sawa na Swalah Khamsini zile za mwanzo?

 

Ibn Hibbaan anasema katika Swahiyh yake (1/133): “Kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifaradhishiwa Swalah Khamsini, amri hii ilikuwa ni mtihani mkubwa, mtihani ambao alitaka kumpima nao kipenzi Wake Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Wakati akimwambia kuwa Ummah wake wakaswali Swalah Khamsini alikuwa anajua fika kuwa wataswali Swalah tano tu na amri ya kuswali Swalah Khamsini ilikuwa ni mtihani tu! Hii ni sawa na maneno yetu kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anaweza Akaamrisha kitu kwa mja Wake ambaye atapokea amri hiyo lakini si lazima aitekeleze kwa vitendo. Mfano mzuri wa hilo ni pale Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alipomwamuru Ibraahiym (‘Alayhis-Salaam) kumchinja mwanae mpenzi. Utashi wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa amri hii ilikuwa ni kuwa Amri Yake ipokelewe na ikubaliwe kikamilifu. Na pindi wote mzazi na mtoto waliposalimu amri na kujisalimisha kwa Mola wao, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alitoa kafara ya mtoto huyo badala yake kwa kafara kubwa sana. Kama Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Angelikuwa Anataka yatekelezwe yale aliyoyaamuru basi Ibraahiym angelikuta mtoto wake kachinjwa kweli. Hali kadhalika kutoa amri ya kuswali Swalah Khamsini kwa kila siku ilikuwa ni amri ya kukubaliwa lakini kitu kingine ambacho ni chepesi kwa matendo chenye uzito sawa sawa ndiyo kifanyike ambazo ni Swalah tano”.

 

Yeyote anayedharau Swalah, siyo kwamba kakataa nguzo ya Uislamu bali pia kakataa zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala). Swalah ni nguzo ya kwanza katika mpangilio aliowekewa binadamu na ndio ibada ya kwanza kuulizwa mja siku ya Qiyaamah na pia ilikuwa ni amri ya mwisho ambayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiitamka mpaka mwisho. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa katika maradhi yake ya mwisho alikuwa akisema: Swalah, Swalah na vile ambavyo mikono yenu ya kuume inavimiliki. [Hadiyth Swahiyh imesahihishwa na Imaam Al-Albaaniy, Ibn Maajah na Musnad ya Ahmad]. Mtu anapokufa hasemi ila maneno yale ambayo anayaona kuwa ni ya muhimu sana kwake na anapendelea watu wachukue ushauri wake wa mwisho. Hivyo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituamuru kwa maneno hayo ambayo aliyaona kuwa ni ya muhimu sana “Tuchunge Swalah”.

 

‘Abdullaah bin Qart alisema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Tendo la kwanza ambalo mja atawajibika nalo siku ya Qiyaamah ni Swalah. Kama Swalah yake itakuwa ni nzuri basi matendo mengine yote yatakuwa ni mazuri. Na kama Swalah itakuwa ni mbaya basi matendo mengine nayo yatakuwa ni mabovu.” [At-Twabaraaniy]

 

Alisema Abu Buraydah bn Al-Haasib: “RasuluLlaah amesema: “Kitu ambacho kinatutofautisha Waumini na makafiri na wanafiki ni jinsi tulivyo karibu na Swalah. Mtu asiyeswali anaangukia katika kundi la makafiri.”  [At-Tirmidhiy Namba 1083]

 

Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema kuwa watu wa motoni watatupwa katika Jahanamu na wataulizwa: Kitu gani kimekusababisheni kuingia katika Moto wa Jahanamu? Nao watajibu,“Hatukuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakiswali.” [Al-Mudathir 74:42-43]. Hivyo jambo la kwanza ambalo wataungama itakuwa ‘walikuwa wameacha Swalah’.

 

Umuhimu wa Swalah unaonekana katika Msikiti wa Qubaa. Msikiti huu ulijengwa wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipohama kutoka Makkah kwenda Madiynah. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikaa sehemu za Qubaa siku nne kabla hajaingia mjini Madiynah, hakupanga kukaa Qubaa wala hakujenga chochote hapa. Kitu alichofanya hapa alijenga msikiti wa Qubaa. Kitendo cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kujenga msikiti hapa Qubaa kinaonesha umuhimu wa Msikiti katika Uislamu. Hivyo basi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipeleka kikundi cha Maswahaba kwenda kupigana Jihaad. Aliwaambia waahirishe vita hivyo, waache kila kitu wakisubiri adhana. Anasema Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu), “Daima mtu alipotoka nasi kwenda kupigana Jihaad dhidi ya watu wowote wale, hakuturuhusu kupigana hadi asubuhi na atasubiri kusikiliza kama kutatokea adhana. Akisikia adhana basi ataahirisha vita hivyo na kama hakusikia adhana basi aliamuru vita hivyo viendelee…”  [Al-Bukhaariy Juzuu 1 Namba 584]

 

Ndugu Waislam, tusome tukio hili kwa mazingatio makubwa kwa kuyafanyia kazi mafunzo yanayopatikana ndani yake, na si kwa kukisherehekea, kufunga na kutenga siku maalum ya kula, kuswali Swalah za aina fulani na du’aa za namna fulani, kugawa vyakula na kufanya mikusanyiko ya masimulizi ya kuburudisha kama ambavyo imekuwa ni ada kwa baadhi ya watu, hayo yote hayajathibiti wala kufanywa na wema waliopita. Tuige matendo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na watangu wema na tutafanikiwa inshaAllaah.

 

 

Vitabu vya Rejea:

Tafsiyr ya Ibn Kathiyr

Swahiyh Al-Bukhaariy

Swahiyh Muslim

Sunan Abu Daawuud

Kitabu cha Siyrah Ar-Rahiyqul-Makhtuum

Mihadhara juu ya Mi’iraaj ya Ihsaan Ilaahi Dhwahiyr.

 

 

Wa biLlaahi At-Atawfiyq

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s