Ahlus Sunnah wal Jama’ah Ni Nini? Ipi Historia Yake Na Malengo Yake? Na Zipi Kasoro Zake?

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunakushukuru ndugu muulizaji kwa swali lako hili zuri na muhimu, nasi tutajitahidi kukujibu kwa kadiri tutakavyowezeshwa na Allaah.

Maana ya Ahlus Sunnah wal Jama’ah

 

Maana ya Ahlus Sunnah wal Jama’ah ni neno la kiarabu lenye kukusanya majina mawili, kwanza ni Sunnah na pili ni Al-Jama’ah, ambayo yote mawili yanatafsirika kilugha kama ifuatavyo:

a.       As-Sunnah: maana yake ni njia, na hapa inamaanisha kufuata na kuchukua yote yaliothibiti kutoka kwa Mtume Muhammad  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutokana na kauli zake, au matendo yake, au kukiri kwake, kwa dhahiri na siri.

b.       Al-Jama’ah: Maana yake kilugha ni idadi yenye wingi, na wametofautiana wanazuoni wa Kiislamu kuhusu maana yake kisheria; baadhi ya wanazuoni wanasema kuwa Al-Jama’ah ni Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wengine wakasema kuwa ni Wanazuoni wa Kiislamu, kama alivyosema Imaam At-Tirmidhiy ” Tafsiri ya neno Al-Jama’ah kwa wanazuoni wa sheria ni wataalamu wa Fiqhi (elimu ya sheria za Kiislamu) na wanazuoni wa Hadiyth (maneno yaliyothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na wengine wakasema Al Jama’ah ni wale walioshikama na haki, hata kama watakuwa wachache, kama alivyosema Ibn Masu’ud ” Al-Jama’ah ni wale walioafikiana na haki hata kama watakuwa peke yako. Na baadhi ya wanazuoni wakasema Al-Jama’ah ni kundi kubwa la watu walio chini ya kiongozi anayehukumu kwa mujibu wa sheria za Allaah na kujiepusha na matamanio na mambo ya uzushi.

Kadhalika ibara Ahlus Sunnah wal Jama’ah ni Watu wa Sunnah na Jama’ah (kikundi). Kusudio la hilo ni wale watu wanaofuata vilivyo njia ya Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) kuhusiana na Imani, Itikadi, amali na utekelezaji wa kijumla wa Dini ya Kiislamu.

Na kauli yenye nguvu miongoni mwa tafsiri hizo, ni mkusanyiko wa yote yalioanishwa na wanazuoni wetu, kwa maana kuwa, Al-Jama’ah ni Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambao ndio kioo na kielelezo cha Manhaj ya Uislamu iliyo safi, aidha wao ndio wanazuoni na wataalamu wa Sheria na Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Vilevile ndio kundi la Waislamu liliokuwa chini ya kiongozi mmoja anayeongoza kwa mujibu wa sheria za Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala). Na Imaam Ibn Hazm amefupisha maelezo haya kwa kusema “Ahlus-Sunnah ambao tunawazungumzia ndio watu wanaofuata haki, na kinyume chao ni watu wanaofuata mambo ya uzushi, hao (Ahlus-Sunnah) ndio Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na ndio wale waliofuata nyayo za Maswahaba katika kizazi cha (At-Taabiu’un) watoto na wafuasi wa Maswahaba wa Mtume, kisha ndio watu wa Hadiyth, na waliowafuata miongoni mwa wanazuoni wa Fiqhi (elimu ya sheria za kiislamu), kizazi kwa kizazi hadi zama tulizonazo hivi sasa.” Angalia kitabu cha Al-Milal wal Ahwa’a wan-Nihal 2/271

Majina mengine ya Ahlus Sunnah Wal Jama’ah:

Aidha Ahlus Sunnah wal Jama’ah wanafahamika kwa majina mengine ambayo yamebeba sifa zao, na ambayo yanatokana na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Miongoni mwa majina hayo ni:

Al-Firqat an-Naajiyah: (kundi litakalookolewa na moto):

Na sifa ya kundi hili imeelezwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Amru bin Al-‘Aaswamesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

ليأتيَنَّ على أُمَّتي ما أتى على بني إسرائيلَ حَذْوَ النعل بالنعل، حتى إن كان منهُم مَن أتى أُمَّه علانية؛ لكان في أُمَّتي مَن يصنع ذلك، وإنَّ بني إسرائيل تفرَّقت على ثنتين وسبعين ملَّة، وتفترق أُمَّتي على ثلاث وسبعين ملة؛ كلهم في النار؛ إلا ملة واحدة. قالوا: ومَن هي يا رسول الله؟ قال: ما أنا عليه وأصحابي ) رواه الترمذي وحسنه الألباني

“Zitawafikia Ummah wangu zama zilizowafikia banu Israaiyl unyayo kwa unyayo, hata kama mtu atamuingilia mama yake hadharani, basi atapatikana miongoni mwa Ummah wangu atakaeigiza hivyo, hakika banu Israaiyl wamafarikiana katika matapo sabini na mbili, na Ummah wangu watafarikiana katika matapo sabini na tatu, wote wataingizwa motoni, ila tapo moja. Wakasema: ni tapo gani hilo ewe Mjumbe wa Allaah? akasema; ni wale ambao watakuwa kama nilivyo mimi na Maswahaba zangu” [At-Tirmidhiy imesahihishwa na Al-Abaaniy]

At-Twaaifat al-Manswuurah: (Kundi lilionusurika):

Kundi hili limetokana na maelezo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pale alipolisifia kwa kusema:

( لا تزال طائفة من أمتي قائمون بأمر الله لا يضرهم من خذلهم أو خالفهم حتى يأتي أمر الله وهم ظاهرون على الناس ) رواه مسلم في صحيحه،

“Halitoacha kundi katika Ummah wangu, wakisimamia maamrisho ya Allaah, hawaathiriwi na wanaowapinga au kuwakhalifu mpaka Allaah Atakapoleta amri Yake, nao watakuwa juu ya watu (wote)”[Muslim]

As-Salaf asw-Swaalih (Waja wema waliotangulia):

Na kundi hilo limeitwa hivi kwa sababu ya kufuata nyayo za Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maimamu waongofu katika karne tatu bora ambazo zilisifiwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ni zama bora kuliko zama zote baada yao, kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

( خيركم قرني ثم الذين يلونهم ثم الذين يلونهم ) رواه البخاري ومسلم  .

“Wabora wenu ni wale wa karne yangu, kisha wale ambao wanaowafuata, kisha wale ambao wanaofuatia” [Al-Bukhaariy na Muslim]

Historia ya Ahlus Sunnah wal Jama’ah

Ama kuhusu historia yake ipo wazi kwani ilianzia wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alikuwa akiwahimiza Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) wawe ni wenye kufuata vilivyo Uislamu kama alivyoteremshiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Kufuata Uislamu kikamilifu ni kufuata Qur-aan na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama tutakavyoona katika dalili zifuatazo:

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema: “Enyi mlioamini! Ingieni katika Uislamu kwa ukamilifu, wala msifuate nyayo za Shetani; hakika yeye kwenu ni adui aliye wazi” [2: 208]

Inafahamika kuwa wanadamu, Waislamu wakiwa miongoni mwao kwa wakati mmoja au mwengine wanakengeuka na msimamo wa sawa. Ili kuubakisha Uislamu katika utwahara wake, Amekuwa (Subhaanahu wa Ta’ala) Akileta kila karne mwenye kujadidi (kuifufua na kuelekeza watu kati njia ya sawa) Dini. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah Anatuma kwa Ummah huu mbele (katika) ya kila karne mwenye kuijadidisha Dini kwao” (Abu Daawuud, al-Haakim, al-Baghdaadiy na al-Bayhaqiy).

Na pia kasema, “Kutabaki katika Ummah wangu kipote kitakachosimama kwa amri za Allaah. Hawatawadhuru wenye kuwaacha wala wenye kuwapinga mpaka ije amri ya Allaah wakiwa katika hali (msimamo) hiyo hiyo” (al-Bukhaariy).

Misingi ya Itikadi (‘Aqiydah) ya Ahlus Sunnah wal Jama’ah:

Itikadi (‘Aqiydah) ya Ahlus Sunnah wal Jama’ah inasifika kwa sifa zifuatazo:

1.       Chimbuko moja la Sheria: Ahlus Sunnah hawategemei chanzo kingine katika misingi ya Itikadi yao zaidi ya Qur-aan, Sunnah na makubaliano ya waja wema waliotangulia, wala hawapingani na yaliyothibiti katika vyanzo hivyo kwa kutumia Qiyaas (kipimo cha akili) au rai.

2.       Kuafikiana kwao na dalili sahihi kunakubaliana na maumbile, akili, na mapokeo: kwani hakuna kinachotuliza nyoyo, zaidi ya Itikadi ya waja wema waliotangulia.

3.       Itikadi ya Ahlus Sunnah iko wazi na nyepesi kueleweka: Ni Itikadi iliyo nyepesi kufahamika kwa watu wa aina zote, isiyokuwa na mafumbo wala mizunguko.

Malengo ya Ahlus Sunnah wal Jama’ah

Ama malengo yake kwa sasa ni kuwarudisha Waislamu katika kufuata kikamilifu Uislamu (Qur-aan na Sunnah) na kuwatoa katika shirki, uzushi na kufuata matamanio ya nafsi zao.

Ikiwa mtu atasema kuwa Ahlus Sunnah wal Jama’ah ni Uislamu wenyewe hatakuwa na makosa wala kasoro yoyote. Na kila Muislamu ni lazima awe na Itikadi hiyo kwa ubora wa Uislamu na ukamilifu wake. Hata hivyo, kwa sababu Uislamu unaelezwa na wanazuoni kuanzia wale wa awali huenda wao wakakosea kwa kutumia dalili (hasa Hadiyth) ima dhaifu, au ya kutungwa, au kukosa kupata iliyo sahihi au kutopata Hadiyth kabisa na hivyo kutumia ijtihadi yake mwenyewe. Ni kwa ajili hii ndio utapata tofauti katika mas-ala tofauti ya Fiqh baina ya Maimamu kwa mfano Abu Haniyfah, Maalik, ash-Shaafi’iy, Ahmad bin Hanbal na wengineo.

Sifa muhimu za Ahlus Sunnah wal Jama’ah

Pamoja na vigezo hivyo, vilevile Itikadi ya Ahlus Sunnah wal Jama’ah inasifika kwa sifa muhimu zifuatazo:

 1. Iymaan isiyokuwa na shaka ndani yake kuwa; Mwenyezi Mungu ni mmoja Hana mshirika, Hafanani na chochote.

 

 1. Iymaan isiyokuwa na shaka ndani yake juu ya majina na sifa za Allaah Subhanahu wa Ta’ala.

 

 1. Kuthibitisha majina na sifa alizozithibitisha Allaah (Subhanahu wa Ta’ala) kwa nafsi Yake, na zikathibitishwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bila kubadilishwa, au kuharibiwa, au kufananishwa, au kuhojiwa.

 

 1. Iymaan isiyokuwa na shaka kuwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni mja wa Allaah na Mtume Wake, na ndio Mtume wa mwisho na Imaam wa wacha mungu na kipenzi cha Allaah.

 

 1. Iymaan isiyokuwa na shaka juu yake juu ya nguzo sita za Iymaan.

 

 1. Iymaan isiyokuwa na shaka ndani yake kuwa, moto na pepo ni viumbe vya Allaah vilivyokwishaumbwa, havimaliziki wala kuangamizwa, na kwamba Allaah Ameumba moto na pepo kabla ya viumbe vingine na kuwaumbia watu Wake, kwa mwenye kuamini na kutenda matendo memo Allaah Atamuingiza katika pepo kwa fadhila Zake, na atakaye kufuru Atamuingiza katika moto kwa uadilifu Wake.

 

 1. Iymaan isiyokuwa na shaka ndani yake, kwa waumini watamuona Mola wao peponi kama ilivyobainishwa na Qur-aan na Sunnah, Allaah Anasema:

{وجوه يومئذ ناضرة إلى ربها ناظرة}

{Zipo nyuso siku hiyo zitazong’ara, Zinamwangallia Mola wao Mlezi.} Al-Qiyaamah: 22-23

 

Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

وقال صلى الله عليه وسلم : ( إنكم سترون ربكم ) رواه البخاري ومسلم

“Hakika ninyi mtamuona Mola wenu) [Al Bukhaariy na Muslim]

 

 1. Kuwa na Itikadi ya kuwa haijuzu kumshuhudilia Muislamu mwenzako kuwa ni mtu wa peponi au wa motoni isipokuwa yule ambae Aayah ya Qur-aan imemshuhudilia hivyo, pamoja na kutaraji malipo mema kwa watendao mema, na kutaraji msamaha kwa wenye makosa.

 

 1. Kuamini kuwa wenye madhambi makubwa ni miongoni mwa Ummah wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hawataadhibiwa milele motoni pindi wakifa hali ya kuwa wanampwekesha Allaah, hata kama watakuwa hawajatubu, na watakuwa baina ya matakwa ya Allaah na hukmu Yake, akitaka Atawasamehe kwa fadhila Zake, na Akitaka Atawaadhibu motoni kwa uadilifu Wake, kisha Atawatoa kwa huruma Yake na kwa kuombewa na waombezi miongoni mwa waja wake watiifu na kuwaingiza peponi.

 

 1.  Hawasimami dhidi ya viongozi wa Kiislamu, muda wa kuwa wanasimamisha hukumu kwa Qur-aan na Sunnah, wala hawavunji utiifu, na wanaamini kuwa kuwatii viongozi wanaohukumu kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah ni katika kumtii Allaah na Mtume Wake.

 

 1.  Wanawapenda Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bila kupunguza mapenzi kwao wala kupituka mipaka katika kuwapenda.

 

 1.  Wanaamini kuwa, Ukhalifa baada ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni wa Abu Bakar, kisha ‘Umar bin al-Khattwwaab, kisha ‘Uthmaan bin ‘Affaan, kisha ‘Aliy bin Abi Twaalib.

 

 1.  Kuamini alama za Qiyaamah, kama vile kuchomoza kwa Dajjaal, na kushuka kwa Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) na kuchomoza jua kutoka upande wa Magharibi na mengine yaliyobainishwa na Hadiyth sahihi.

 

Baadhi ya Maimamu wa Ahlus Sunnah wal Jama’ah

 1. Kiongozi mkuu na Imaam wa kwanza kabisa wa Ahlus Sunnah wal Jama’ah ni Muhammad bin Abdillaah bin ‘Abdil-Muttwwalib (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
 2. Kisha wanafuatia Makhalifa waongofu, nao ni:

Abu Bakar As-Swiddiyq

‘Umar bin al-Khattwwaab

‘Uthmaan bin ‘Affaan

‘Aliy bin Abi Twaalib

 1. Kisha wanafuatia Maswahaba watukufu na waliowafuata baada yao ambao wameacha athari kubwa kama:

Abu Haniyfah An-Nu’maan

Abu Abdillaah Maalik Bin Anas

Muhammad bin Idriys Ash-Shaafi’iy

Ahmad bin Muhammad bin Hanbal

 1. Na wengineo ambao pia wameacha elimu kubwa sana katika Ummah huu kama:

Abu ‘Abdillaah Muhammad bin Isma’iyl bin Ibraahiym bin al-Mughiyrah bin Bardizbah al-Bukhaariy

Abu al-Husayn Muslim bin al-Hajjaaj bin Muslim al-Qushayriyy an-Naysaabuuriyy, Muslim

Abu Al-‘Abbaas Ahmad bin ‘Abdil-Haliym, Ibn Taymiyah

Muhammad bin Abi Bakr bin Sa‘ad, Shamsud-Diyn, Abu ‘Abdillaah al-Zur‘i ad-Dimashqiy al-Hanbali, Ibn Qayyim al-Jawziyyah

Muhammad bin Ahmad bin ‘Uthmaan bin Qaymaz, Abu ‘Abdillaah Shamsud-Diyn adh-Dhahabiy

Abu Al-Fidaa, ‘Imadud-Diyn Isma’iyl bin ‘Umar, Ibn Kathiyr

Abu Zakariyha Muhyud-Diyn Yahya bin Sharaf An-Nawawiy

‘Al-Haafidh Shihabud-Diyn Abul-Fadhwl Ahmad bin ‘Aliy bin Muhammad, Ibn Hajar al-‘Asqalaaniy

Abu Ja’afar Ahmad bin Muhammad bin Salaamah bin Salama ‘Abdil-Maalik bin Salama Al-Azdiy Atw-Twahaawiy

Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab at-Tamiymiy

Muhammad bin ‘Aliy ash-Shawkaaniy

Na wengi wengine ambao hatuwezi kuwataja wote hapa.

Ndugu muulizaji kataka kujua kasoro za Ahlus Sunnah, tunamjulisha kuwa Itikadi yenyewe kama tulivyoieleza juu ni kuwa ni itikadi ya wema waliotangulia na inafuata yale yote aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bila kupunguza wala kuongeza chochote. Kasoro si katika itikadi, bali kasoro huenda zikapatikana kwa baadhi ya wale wanaodai kuwa wao ni Ahlus Sunnah na huku wakizusha mambo katika Dini, wakifanya shirki, wakitanguliza akili zao mbele ya Qur-aan na Sunnah, na huku wakidai kuwa wao wanafuata ‘Aqiydah ya Ahlus Sunnah wal Jama’ah. Na ndio leo hii utaona kila mtu anadai yeye ni Ahlus Sunnah lakini anaweza kuwa yale anayoyafuata au kuyaamini ni kinyume kabisa na Ahlus Sunnah wal Jama’ah.

Kwa mukhtasari hii ndio Ahlus Sunnah wal Jamaa’ah

Na Allaah Anajua Zaidi

Advertisements

One response to “Ahlus Sunnah wal Jama’ah Ni Nini? Ipi Historia Yake Na Malengo Yake? Na Zipi Kasoro Zake?

 1. JazzakaALLAH kheir

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s