Nyakati Tatu Muhimu Za Kufanya Ibada – Zisikupite Katika Ramadhaan

Nyakati tatu hizi ni muhimu sana za kufanya ibada kutokana na fadhila zake kuu. Mwenye kupenda kuchuma thawabu nyingi asizikose khaswa katika mwezi huu Mtukufu Wa Ramadhaan ambao ni mwezi wenye malipo maradufu

1-Wakati wa mwanzo:  Baina ya Alfajiri na jua kuchomoza:

Usimulizi uliothibiti kutoka katika Swahiyh Muslim (564/1) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba walikuwa wakibakia macho wakati huo hadi jua kuchomoza kwani ni wakati mja anapogaiwa rizki yake, na ni wakati wenye kheri nyingi, unampa siha nzuri ya mwili binaadamu, na kwa ujumla ni wakati wenye baraka nyingi za kila aina kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliomba:

((اللهم بارك لأمتي في بكورها))  الترمذي, أحمد, أبي داود, ابن ماجه

((Ewe Allaah, wabarikie Ummah wangu nyakati za asubuhi mapema))[At-Tirmidhiy, Ahmad, Abu Daawuud, Ibn Maajah na imethibitishwa kuwa ni Hadiyth Swahiyh na Shaykh Al-Albaaniy]

Usimulizi huu umetoka kwa Maswahaba kadhaa ambao wameelezea kwamba: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipotaka kupeleka kikosi au jeshi aliwapeleka mwanzo wa asubuhi”. Vile vile wamesimulia kwamba: “Swakhar alikuwa mtu tajiri ambaye alikuwa akipelekea biashara zake mwanzo wa asubuhi na matokeo yake ilikuwa ni kufuzu katika biashara na kupata faida kubwa sana”.

Wamesimulia Salafus-Swaalih kwamba Ibn ‘Abbaas naye alimkataza mtu kulala nyakati hizo alipomwambia:

   “قُم، أتنام في الساعة التي تقسَّم فيه الأرزاق؟”

“Inuka! Je, unalala katika saa ambayo rizki inagaiwa?”

Ikiwa basi wakati huo ni kama hivyo ilivyoelezwa juu, basi vipi Muislamu auache wakati huu umpite khaswa katika mwezi huu mtukufu wa Ramdhaan?

Ibnul-Qayyim (Rahimahu-Allaah) katika kitabu chake ‘Zaad Al-Ma’aad‘ amesema: “Usingizi wa asubuhi unanyima rizki kwani huo ni wakati ambao Muumba anaombwa rizki na wakati wa kugaiwa rizki. Hivyo usingizi unanyima rizki isipokuwa kwa dharura. Usingizi wakati huo pia ni madhara kwa mwili…”

 

Faida nyingine kubwa ya kubakia macho ukimdhukuru Allaah wakati huu:

Si chini ya muda wa saa na nusu utakuwa umepata thawabu za Hajj na ‘Umrah kamilifu:

عن أنس عن النبي صلى الله عليه وسلم ، أنه قال  (( من صلى الفجر في جماعة ثم قعد يذكر الله  حتى تطلع الشمس ثم صلى ركعتين كانت له كأجر حجة وعمرة تامة تامة تامة) ) أخرج الترمذي  صححه الألباني .

Imetoka kwa Anas kwamba Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayeswali Alfajiri katika Jama’ah kisha akakaa anamkumbuka Allaah mpaka likachomoza jua kisha akaswali Raka’ah mbili, atapata ujira kama ujira wa kwenda Hajj na ‘Umrah ulio kamili kamili kamili)) [Imetolewa na At-Tirmidhiy na kaisahihisha Al-Albaaniy]

 

 

Pindi ukifanya hivyo kwa mwezi mzima utakuwa umechuma thawabu za Hajj na ‘Umrah mwezi mzima. Hizo ni fadhila za siku za kawaida, seuze ukifanya mwezi mtukufu huu wa Ramadhaan? Jitahidi ndugu Muislamu kadiri uwezavyo kuchuma hizi thawabu kubwa ambazo zingelikukalifu mali, tabu za safari na mashaka ya kufika Makkah kutekeleza ibada hizo. Lakini kwa Rahma ya Allaah Ametujaalia tuweze kuzichuma tukiwa majumbani mwetu tena kwa wepesi kabisa. Wanaume thawabu zitazidi ikiwa watatekeleza wakiwa misikitini. Wanawake wanazipata fadhila hizo hata wakiswali majumbani mwao.  Hata hivyo, pamoja na ujira wote huu, tusisahau kuwa fadhila hizo hazivunji wala hazifuti fardh ya kwenda Hajj kwa mwenye uwezo, asije mtu akadhani kufanya hayo kutakuwa kumetengua wajiibu wake wa kuhiji au kufanya ‘Umrah.

 

 

 

 

 

2- Wakati wa pili: Kabla ya Jua kuzama (Magharibi):

 

Huu ni wakati ambao bado Muislamu yuko katika Swawm na du’aa yake anayoiomba hairudi:

 

 قال صلى الله عليه وسلم: ((ثلاثة لا ترد دعوتهم: الصائم حتى يفطر والإمام العادل والمظلوم))  وروى الترمذي  بسند حسن

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (([Watu] watatu du’aa zao hazirudi; mwenye kufunga hadi afuturu/afutari, Kiongozi muadilifu na aliyedhulumiwa)) [At-Tirmidhiy kwa isnaad nzuri]

 

 

Kwa hiyo ni fursa ya kuitumia Muislamu aombe du’aa na haja zake wakati huu khaswa pia kwa vile ni wakati ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amehimiza Atukuzwe kamaAnavyosema:

 

 (( وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ الْغُرُوبِ))   

((.. na mtakase kwa kumsifu Mola wako  kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa)) [Qaaf: 39]

 ((وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ غُرُوبِهَا وَمِنْ آنَاء اللَّيْلِ فَسَبِّحْ وَأَطْرَافَ النَّهَارِ لَعَلَّكَ تَرْضَى))

((…Na umtakase Mola wako kwa kumsifu kabla ya kuchomoza jua, na kabla halijachwa, na nyakati za usiku pia umtakase, na ncha za mchana ili upate ya kukuridhisha)) [Twaahaa: 130].

 

 (( وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ بِالْعَشِيِّ وَالْإِبْكَار))  

((…Na omba msamaha kwa dhambi zako, na umtakase Mola wako  kwa kumhimidi jioni na asubuhi)) [Ghaafir: 55]

3- Wakati wa tatu: Suhuur – Kabla ya Alfajiri

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amewaaahidi Wacha Mungu Pepo kwa sababu sifa mojawapo yao ni kuomba maghfira kabla ya Alfajiri:

 

 إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُون)) ((آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَلِكَ مُحْسِنِينَ))  ((كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ))  ((وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُون))

((Hakika wenye taqwa watakuwa katika Mabustani na chemchem)) ((Wanapokea Aliyowapa Mola wao. Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema)) ((Walikuwa wakilala kidogo tu usiku)) ((Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfira)) [Adh-Dhaariyaat: 15-18]

 

 

 

Kisha wamesifiwa tena kwa sifa hiyo hiyo pamoja na nyinginezo:

 

((الصَّابِرِينَ وَالصَّادِقِينَ وَالْقَانِتِينَ وَالْمُنفِقِينَ وَالْمُسْتَغْفِرِينَ بِالأَسْحَارِ))  

 

((Wanaosubiri, wanaosema kweli, na watiifu, na wanaotoa sadaka, na wanaoomba maghafira kabla ya Alfajiri)) [Al-‘Imraan: 17]

 

Muislamu asiache wakati huo umpite kwani ni wakati muhimu na wenye fadhila na faida kubwa kwa vile Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Huteremka wakati huo kutoka mbingu ya saba na kuweko mbingu ya ardhi kutukidhia haja zetu:

 

 عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((ينزل ربنا تبارك وتعالى كل ليلة إلى السماءالدنيا حين يبقى ثلث الليل الآخر فيقول: من يدعوني فأستجيب له؟ من يسألني فأعطيه؟ من يستغفرني فأغفر له )) البخاري و مسلم

Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia (mbingu ya kwanza) inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba Nimtakabalie? Nani ana shida Nimtekelezee? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

Nani miongoni mwetu asiyemhitaji Mola wake kumkidhia haja zake na kumuondeshea shida zake? Nani asiyekuwa na madhambi asiyemhitaji Mola wake kumghufuria? Hivyo usiache wakati huu ukakupita khaswa kwa vile mwezi huu Mtukufu ambao kila jambo ulifanyalo lina fadhila na thawabu marudufu.

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atuwezeshe kudiriki nyakati hizo tatu na nyingine, tuwe katika ibada katika mwezi huu wa Ramadhaan na miezi yote mingineyo na Atujaalie kheri na Baraka nyingi, Atukidhie haja zetu, Atuondoshee shida zetu na Atughufurie madhambi yetu yote. Aamiyn.

2 responses to “Nyakati Tatu Muhimu Za Kufanya Ibada – Zisikupite Katika Ramadhaan

  1. inshallah mungu awalipe

  2. inshallah nawatakia kila la kheir na afya njem mwenyezimungu sub hana wataala atawalipa

Leave a reply to Hassan Rajabu Cancel reply